UNCDF YAISAIDIA ENSOL KUPELEKA UMEME VIJIJINI

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Mitaji na Maendeleo (The United Nations Capital Development Fund-UNCDF), ikishirikiana na kampuni ya Ensol Tanzania Ltd. (Ensol) wamezindua mfumo wa umeme wa nishati ya jua katika kijiji cha Mpale kilichopo wilaya ya Korogwe, na hivyo kuwezesha umeme katika eneo hilo kwa mara ya kwanza.

Mradi huo ulizinduliwa rasmi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dk. Juliana Pallangyo ambaye aliipongeza kampuni ya Ensol na washirika wake ikiwemo UNCDF kwa juhudi zake kubwa za ushawishi wa umeme hasa umeme mbadala wa jua ili kuboresha ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa mtu binafsi na taifa.

Dk. Pallangyo alisema kwamba serikali ya Tanzania inawashukuru watu wa Ensol kwa juhudi zao kubwa za kupeleka umeme vijijini.

Alisema kwa Ensol kuweza kufikisha umeme katika maeneo ya ndani kabisa ya kijiji cha Mpale, kuwaunganisha wananchi na umeme wa saa 24 na wamefanikiwa kubadili maisha ya wananchi hao.

Alitoa wito kwa jumuiya hiyo kutumia umeme sio kwa kuwasha taa pekee bali pia katika kusukuma mbele kazi za uzalishaji.

Dk. Pallangyo alifurahishwa na kituo cha afya Mpale kuunganishwa na mfumo wa nishati ya jua na kuwataka maofisa wa wilaya kulipa Ankara zao kwa wakati ili kuhakikisha kwamba huduma zinapatikana bila kukoma kwa wananchi. 

Kijiji cha Mpale kipo katika maeneo ya milimani katika kata ya Mpale wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. Kijiji chenye wakazi 9000 na nyumba 730, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1972 hakijawahi kuwa na umeme.

Wengi wa wanavijiji walikuwa wakitegemea mno mafuta ya taa ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa si masafi kwa ajili ya kuwashia taa zao.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Juliana Pallangyo akitoa nasaha wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga. Kulshoto ni Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Mitaji na Maendeleo (UNCDF), Peter Malika.
Mpaka sasa Ensol imeshaunganisha umeme kwa kaya 50. Aidha mpango unafanyika wa kutanua mradi ili ifikapo Juni 2018 nyumbna 250 ziwe zimeunganishwa.

Mreadi huo wa kuunganisha wanakijiji na nishati inayozalishwa kwa nguvu za jua ulianza mwaka 2014 wakati Ensol walipozuru vijiji kadhaa vya mkoa wa Tanga kuangalia uwezekano wa kupata kijiji cha mfano na kubaini kuwapo kwa kijiji cha Mpale.

“Ushirikiano wa UNCDF ulikuwa muhimu katika mradi huu gridi ndogo ya nishati ya jua. Pamoja na kwamba tulipokea fedha kutoka UNCDF na wadau wengine, UNCDF imekuwa ndio chombo cha kuingiza masuala ya kitaalamu na ushauri mwingine. Kushirikiana na UNCDF kumeongeza kuaminika miongoni mwa wadau na taasisi za kifedha,” anasema Prosper Magali, Meneja wa mradi wa Mpale.
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Mitaji na Maendeleo (UNCDF) nchini, Peter Malika akizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa rasmi wa mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale, wilayani Korogwe mkoa wa Tanga.

Bw. Magali aliongeza, “Ninaamini kama si msaada wa UNCDF huu mradi usingekuwepo hapa ulipo. Tumepokea fedha kutoka EEP na wafadhili wengine. Lakini ni kwa sababu ya UNCDF tumeweza kupata fedha kutoka katika taasisi nyingine za ufadhili”.

Mkuu wa UNCDF Tanzania, Peter Malika alisema kwamba umeme ni chanzo cha maendeleo na kwamba sekta binafsi ina nafasi ya kusaidia serikali katika juhudi zake za kuangaza maeneo ya vijijini.

“Kwa kuwezesha Mpale kuwa na umeme tunawasaidia wananchi wa kijiji hiki kufanya maendeleo ya kiuchumi. Fursa nyingi za kiuchumi zitaibuka, kituo cha afya kitaweza kuboresha huduma zake na wanafunzi watakuwa na muda zaidi wa kusoma.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Ensol Tanzania, Hamisi Mikate akielezea mchakato wa kufanikisha mradi huo ulivyoenda mpaka kukamilika wakati wa ufunguzi wa rasmi wa mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale wilayani Korogwe, mkoa wa Pwani.

Mafanikio ya mradi huo ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya serikali ya mitaa na wananchi wakati wote wa mchakato wa kufanikisha mradi.

“Wananchi wamefarijika tangu kampuni ya Ensol itembelee kijiji hicho kwa mara ya kwanza na kuzungumza kuhusu uletaji wa umeme wa nishati ya jua. Tumekuwa na ushirikiano mkubwa tangu siku ya kwanza ambapo wamekuwa wakitushirikisha,” anasema Mwenyekiti wa kijiji Augustine Rugambwa.

Bw.Rugambwa aliongeza: “Nimefurahishwa sana kwamba mradi huu umekuja wakati wa uongozi wangu. Ni nafasi adimu ambayo nitaikumbuka maisha yangu yote. 

Tunawashukuru sana UNCDF kwa kutukumbuka hata sisi tuliopembezoni. Kupitia Ensol tutaingiza nishati ya umeme majumbani mwetu. UNCDF tunawashukuru kwa msaada wenu huu. Kamwe hatutawasahau.”
Mkurugenzi wa Miradi wa Ensol na Meneja wa Mradi wa Umeme Mpale, Prosper Magari akizungumza jambo na kutoa shukrani kwa UNCDF kwa kuwezesha kufanikisha mradi huo wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale, wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga.
“Tunaamini kwa msaada tulioupata kutoka UNCDF na wengine, mradi huu utakuwa endelevu na utakaokuwa unatengeneza faida kwani wateja watakuwa wanalipa Ankara zao kila mwezi. Kwa hiyo fedha zitakazopatikana zitatumika kuufanya mradi kuwa endelevu,” alisema Prosper.

“Tunatumia mradi kama huu kama mafunzo. Lengo letu ni kuwa na miradi mingine kama hii 15 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Tumetembelea maeneo ya nyanda za juu Kusini kuona vijiji vinavyoweza kupatiwa mradi wa umeme wa jua. Tumekubaliana na serikali za mikoa na tawala za mitaa kuwapeleka nishati ya umeme jua na tunatarajia kuwaunganisha na watu nyumba elfu kumi. 

Kuna vijiji vingi kama hiki cha Mpale vinavyohitaji umeme, kwa hiyo fursa za umemejua ni kubwa sana!” aliongeza Prosper.

Bw Malika alisema kwamba UNCDF itaendelea kufanyakazi kwa karibu na Ensol na taasisi nyingine za umma na binafsi kuwezesha kufikisha umeme katika maeneo yanayofikika wka shida nchini Tanzania.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mpale, Augustine Rugambwa akisoma risala fupi kwa mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa rasmi wa mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale uliofanyika mwishoni mwa juma wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga.
Kikundi cha utamaduni Mpale, Millongwe wakitoa burudani wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale, wilayani Korogwe, mkoani Tanga.
Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Juliana Pallangyo (katikati) akishiriki kucheza ngoma ya ‘Mdumange’ ya kabila la Wasambaa wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale, wilayani Korogwe mkoa wa Pwani.
Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Juliana Pallangyo akifunua kitambaa kuzindia rasmi mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga ambao utasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu. Kushoto ni Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Mitaji na Maendeleo (UNCDF), Peter Malika.

Mgeni rasmi na meza kuu wakitazama wakisoma maneno yaliyoaandikwa kwenye kibao hicho baada ya kuzinduliwa rasmi.
Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Juliana Pallangyo katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhiria uzinduzi rasmi mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga.
Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Juliana Pallangyo akibadilishana mawazo na Mkuu wa wilaya ya Korogwe, Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) na Mkurugenzi wa Miradi wa Ensol na Meneja wa Mradi wa Umeme Mpale, Prosper Magari katika chumba maalum cha kusambazia umeme katika kijiji cha Mpale mara kuzindua rasmi mradi huo.
Muonekano wa ndani wa mitambo ya kusambazia umeme kwenye kijiji cha Mpale.
Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Juliana Pallangyo akitembelea chumba cha betri za solar zinazosambaza umeme katika kijiji hicho.
Jenereta la akiba linaloweza kuhudumia kijiji cha Mpale endapo kutatokea hitilafu yoyote.
Mmoja wa wageni walioshiriki uzinduzi huo akipata huduma ya kunyoa ndevu baada mradi huo wa umeme wa nishati ya jua kuzinduliwa rasmi katika kijiji cha Mpale, wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga.
Pichani juu na chini ni sehemu ya viongozi mbalimbali wa serikali, wananchi wa kijiji cha Mpale, wafanyakazi wa ENSOL na UNCDF waliohudhuria uzinduzi rasmi mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga.






Jengo la mradi wa uzalishaji mdogo wa umeme wa 48KW kwa teknolojia ya nishati ya jua katika kijiji cha Mpale wilayani Korogwe, mkoa wa Tanga. Na Zainul Mzige
Powered by Blogger.