Serikali Yaingiza Tani 55,000 za Mbolea Ili Kudhibiti Mfumuko wa Bei
Na. Eliphace Marwa – Maelezo
Serikali
imeingiza nchini jumla ya tani elfu 32 za mbolea ya kukuzia pamoja na
tani elfu 23 za mbolea ya kupandia kupitia mfumo mpya wa uagizaji wa
mbolea kwa pamoja, lengo likiwa ni kudhibiti bei kwa kuzingatia bei
elekezi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam wakati zoezi la upakuaji wa
mbolea hiyo likiendelea Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora
wa Mbolea Tanzania(TFRA) Bw. Lazaro Kitandu amesema kuwa mpaka sasa
jumla ya tani elfu 55 za mbolea zimewasili nchini.
Hii
ni awamu ya kwanza ya kuingiza mbolea nchini kupitia mfumo mpya ya
uagizaji mbolea kwapamoja ambapo kampuni ya OCP S.A ya nchini Morocco
imeingiza jumla ya tani elfu 23 za mbolea ya kupandia na Kampuni ya
Premium Agro Chem imeingiza tani elfu 32 za mbolea ya kukuzia.
“Mpaka
sasa zoezi la kupakua mbolea ya kupandia (DAP) tani elfu 23 linaendelea
vizuri na mara baada ya kumaliza kupakua mbolea hii tutaanza zoezi la
kupakua mbolea ya kukuzia (UREA) ambayo ni tani elfu 32,” alisema Bw.
Kitandu.
Kitandu
aliongeza kuwa Mheshimiwa Waziri wa kilimo juzi alipokuwa anaongea na
waandishi wa habari mjini Dodoma na akasisitiza bei ambazo zimetolewa
zisimamiwe na kila ngazi kwasababu taasisi peke yake haiwezi kuwa na
watu kila mahali hivyo Tawala za mikoa, Serikali za mitaa mpaka Kijiji
zitasaidia kusimamia bei ambazo zimetolewa.
Pia
Kitandu aliongeza kuwa kuhusiana suala la bei ya mbolea hiyo
itatangazwa kupitia vyombo vya habari kama vile magazeti na televisheni
na hivyo kutoa onyo kwa mawakala kujipangia bei kwa kuuza mbolea nje ya
bei elekezi ya Serikali kwamba watachukuliwa hatua za kisheria kama
kunyang’anywa leseni, kufungwa, faini au vyote kwa pamoja.
Aidha
Kitandu alisisitiza kuwa mbolea hizi siyo mbolea za ruzuku kwani
wakulima wengi wamekuwa wakichanganya mbolea hizi na mbolea za ruzuku na
amefafanua kuwa mbolea hii imefanyiwa utaratibu wa kudhibiti toka kule
inapotoka na hivyo serikali itahakikisha mbolea hii inauzwa kwa
kulingana na bei ya soko la dunia.
Aidha
Bw. Kitandu aliwahakikishia wakulima kuwa mbolea itasafirishwa mpaka
vijijini kwa kutumia treni na malori kwa sehemu ambapo treni haiwezi
kufika, na amewatoa hofu wakulima kuwa msimu unaoanza mwezi huu
wameingiza tani 23,000 kwa mbolea ya kupandia (DAP) na tani 32,000 kwa
mbolea ya kukuzia (UREA) ambapo watakuwa wanaagiza kwa awamu kwa miezi
miwili miwili.