Mlinzi wa Meja Jenerali aliyejeruhiwa kwa risasi Dar akamatwa
Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili
akiwemo mlinzi wa Suma JKT na mhudumu wa benki ya NBC tawi la Tangibovu
ambao wanatuhumiwa katika tukio la kujeruhiwa kwa risasi Meja Jenerali
Mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), Vincent Mritaba.
Kamanda
wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema leo Jumatano kuwa Septemba 11
mwaka huu saa 11 jioni maeneo ya Tegeta Masaiti jeshi hilo lilipata
taarifa ya Mritaba kuvamiwa na watu wawili wasiojulikana ambao
walimjeruhi na kumpiga risasi ya begani, tumnoni na kwenye paja la mkono
wa kulia huku wakimpora kiasi cha Sh5 milioni.
Amesema
tukio hilo lilitokea baada ya mstaafu huyo kutoka kuchukua fedha hizo
katika benki ya NBC tawi la Tangibovu akiwa kwenye gari lake ya
Volkswagen Amarok.
Mambosasa amesema alipofika nyumbani kwake alipiga honi na kufunguliwa geti na mlinzi wake Godfrey Gasper.
Amesema
geti lilipofunguliwa pikipiki ilisimama hapo getini na watu wawili
waliokuwa wamevaa helment walishuka na kulifuata gari huku wakiwa na
silaha aina ya bastola ndipo walishambulia upande wa kulia wa dereva na
katika kioo cha mbele.
"Huku
wakimwamuru ashuke ambapo risasi zilimjeruhi maeneo ya begani, tumboni
na kwenye paja la mkono wa kulia na kutokomea kusikojulikana kwa kutumia
pikipiki waliokuja nayo," amesema Mambosasa.
Mambosasa
amesema cha kushangaza wakati mlinzi huyo anaenda kufungua geti silaha
yake aina ya shotgun yenye namba TZCAR9644 aliiacha kwenye kibanda cha
ulinzi huku ikiwa chini ya kitanda.
Amesema
baadaye watuhumiwa walimwambia akimbie katika eneo hilo na yeye alitii
amri hiyo na kwenda mbali na tukio hilo jambo ambalo linatia shaka.
"Ninavyojua
askari wa Suma JKT anapewa mafunzo ya ukakamavu haiwezekani uache
silaha chini ya kitanda unakwenda kufungua geti kitu ambacho sikubaliani
nacho,"amesema
Amesema
walipofuatilia mawasiliano ya mmoja wa wahudumu wa benki hiyo walibaini
kuwa alikuwa anapanga mipango na watu mbalimbali wanaokwenda katika
benki hiyo. Hivyo msako mkali unaendelea ili kuwabaini watuhumiwa
waliohusika katika tukio la kujeruhi kwa risasi afande huyo.
Pia
alizungumzia kuvunjwa kwa ofisi ya wakili ya Prime Attoneys akieleza
kuwa wanaendelea na msako mkali ili kuwabaini waliohusika katika tukio
hilo na watakapokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.