MJI MKONGWE WA ZANZIBAR: PALE DUNIA YA KALE INAPOKUTANA NA YA KISASA
Miongoni mwa majengo yake mengi yakiwa
yamejengwa mnamo karne ya 18 na 19, Mji Mkongwe wa Zanzibar bado
haujapoteza taswira yake halisi mpaka hivi leo. Na kutokana na muonekano
huo, kutembea na kuvinjari mitaa na majengo mbalimbali kunakufanya
ujihisi kama kweli ulikuwepo kipindi cha nyuma pindi inajengwa.
Kati ya majengo maarufu ambayo Jumia
Travel inakuhakikishia utayaona pindi utakapoingia kwenye mji huu ni
pamoja na Ngome Kongwe iliyojengwa kwenye eneo la mwanzo la Kanisa la
Wareno; nyumba ya maajabu; kasri kubwa iliyojengwa na Sultan Barghash;
zahanati ya kale; Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Joseph; Kanisa Kuu la
Kristu la Waanglikana likiwa limejengwa kukumbuka kazi ya David
Livingstone katika kukomesha biashara ya utumwa na kujengwa eneo lilipo
kuwepo soko la watumwa; makazi ya aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa
watumwa Tippu Tip; Msikiti wa Malindi Bamnara; jengo la Jamat Khan
lililojengwa kwa ajili ya dhehebu la Ismailia; eneo la makaburi ya
Kifalme; na mabafu ya Kiajemi.
Kwa pamoja, mitaa na barabara nyembamba
zikiwa na kona nyingi, na majengo makubwa yanayotazamana na bahari ndyo
yanaufanya mji huu kuwa wa kipekee ukiakisi shughuli za muda mrefu za
kibiashara kati ya Waafrika na Waarabu. Kwa ujumla, Mji Mkongwe
unatambulika kama sehemu ambayo hatimaye biashara ya utumwa ilikomeshwa.
Kutokana na upekee na umaarufu wake
mamia ya maelfu ya watalii kutoka kona mbalimbali za dunia husafiri kuja
kujionea vivutio vya kila aina vinavyopatikana kwenye mji huu mkongwe
wa Zanzibar.
Kwa ufupi takribani kila kitu ndani ya
Mji Mkongwe kina historia ya kuvutia na kusisimua. Kuanzia mila na
tamaduni za watu wake, shughuli wanazozifanya, vyakula vyao na majengo
ni utalii tosha ambao hauwezi kupatikana sehemu yoyote duniani.
Huchukua muda wa saa moja na nusu
kusafiri kwa kutumia boti kutoka Dar es Salaam mpaka kufika Zanzibar na
usafiri huanzia saa moja asubuhi mpaka saa 12 za jioni. Hivyo basi kumbe
inawezekana kwa mtu kutokea jijini Dar es Salaam akaenda kule, akatalii
na kurudi siku hiyo hiyo. Na kama una mpango wa kuufaidi zaidi mji huo
pia inawezekana kwani vyakula na malazi vya gharama nafuu kabisa ambayo
kila mtu anaweza akamudu.
Uzuri wa Mji Mkongwe ni kwamba ni rahisi
kuuzunguka kwani mitaa yote inapitika kwa urahisi kabisa aidha kwa
kutumia ramani ya karatasi au simu (google map) au muongozaji wa kitalii
utayempata. Ni vizuri kuwa na muongozaji mzuri kama ni mara yako kwanza
kufika kule ili iwe rahisi na pia kutembelea sehemu nyingi zaidi ambazo
hauzifahamu.
Kikubwa cha kushangaza zaidi ni namna
majengo yalivyojengwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia vifaa mbalimbali
kama vile chokaa, matumbawe na miti. Na cha kuvutia zaidi ni umri wa
majengo hayo ambayo yamekuwepo karne na karne bila ya kupoteza uhalisia
wake. Pongezi kubwa ziende kwa serikali na shirika la Umoja wa Kimataifa
la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuweka jitihada kubwa na
sheria za kuulinda mjii huu. Kutokana na jitihada hizo mnamo mwaka 2000
UNESCO liliutangaza Mji Mkongwe wa Zanzibar kama eneo la urithi wa
dunia.
Utakuwa haujaufaidi Mji Mkongwe endapo
hautopata fursa ya kula vyakula mbalimbali (vya baharini)
vinavyopatikana katika migahawa tofauti. Eneo maarufu ambalo unaweza
kuvipata vyakula vya aina hiyo kwa pamoja ni kwenye bustani ya
Forodhani. Litakuwa jambo la ajabu kama umefika Zanzibar na hukuenda
kutembelea eneo hili. Umaarufu wa bustani ya Forodhani umetokana na
mkusanyiko wake wa aina lukuki za vyakula vya baharini vinavyopatikana
pale kila siku kuanzia jioni. Na ni eneo ambalo huwakutanisha watu
kutokea sehemu mbalimbali za visiwa vya Zanzibar, hivyo inawezekana
kukutana na watu ambao mlikuwa mkipishana mchana kutwa.
Kutembelea, kuogelea na kutazama jua
likizama kwenye fukwe ya bahari ya Hindi ukiwa Zanzibar nazo ni miongoni
mwa shughuli ambazo watalii wengi hufurahia. Baadhi ya hoteli ambazo
ukiwa kwenye Mji Mkongwe unaweza kuyafanya hayo ni kama vile Mizingani
Seafront Hotel, Africa House Hotel na Seyyida Hotel & Spa.
Kwa kumbukumbu zako itakuwa ni vema
zaidi ukibeba kamera kwa ajili ya kupiga picha matukio mbalimbali
unayoyaona njiani. Kwa majengo inakuwa ni rahisi zaidi ila kwa watu
itakuwa ni busara ukaomba ruhusa ili kuepuka matatizo kwani sio wote
watakuwa tayari kufanya hivyo. Zanzibar ni kubwa na ina maeneo mengi ya
kutembelea ila kwa leo Jumia Travel inaamini angalau utakuwa umeipata
picha ya Mji Mkongwe wa Zanzibar na shughuli za kufanya na kufurahia
ukiwa kule.
Na Jumia Travel Tanzania