KATIBU MKUU WA CHADEMA ASIMULIA JINSI ALIVYOHOJIWA NA POLIS
Katibu
Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent
Mashinji amehojiwa na polisi kuelezea namna anavyowafahamu watu
waliofanya shambulio la risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu.
Akizungumza jana baada ya kutoka katika mahojiano hayo na maofisa wa
polisi, Dk. Mashinji alisema maofisa hao walimtaka kuelezea
alichowaambia waandishi wa habari katika mkutano wake nao mara baada ya
kutokea kwa tukio hilo ambapo alionyesha dalili ya kuwafahamu
waliohusika na tukio hilo.
“Niliwataka kurejea kwenye yale mazungumzo ili kuangalia kama nilionyesha dalili ya kuwafahamu watu hao au la.
“Baada ya kuwaambia hivyo walirejea kwenye mazungumzo hayo na kubaini
kuwa katika kauli zangu sikuonyesha kama nilikuwa nawajua watu hao bali
niliwataka wananchi kufufua polisi jamii ambayo itasaidia kuimarisha
ulinzi,” amesema.
Dk. Mashinji amesema kutokana na hali hiyo, maofisa hao wa polisi
walitaka kujua kama anazo taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo ambapo
alijibu hana taarifa hizo ila aliwataka polisi kuhakikisha waliofanya
tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.
Mahojiano hayo ya polisi na Dk. Mashinji, yanatokana na wito wa Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto ambaye alimtaka kiongozi huyo
kufika kwenye Ofisi ya Polisi ya Mkoa wa Dodoma au Ofisi ya DCI kwa
ajili ya mahojiano.