MBUNGE MDOGO ZAIDI KENYA AKABIDHIWA GARI NA RAIS KENYATTA
***
Mbunge wa umri mdogo zaidi nchini Kenya amekabidhiwa gari ambalo alikuwa ameahidiwa na Rais Uhuru Kenyatta.
John Paul Mwirigi, 23, ambaye ni mbunge wa Igembe Kusini, takriban
kilomita 200 mashariki mwa jiji la Nairobi, alichaguliwa akiwa bado
mwanafunzi wa chuo kikuu.
Bw Mwirigi alitumia baiskeli na pikipiki za kusafirisha abiria, maarufu kama bodaboda, kuwafikia watu wakati wa kampeni.
Nyingi za pesa alizotumia wakati wa kampeni alizipokea kutoka kwa wahisani.
Wakati wa kuapishwa, alitumia magari ya uchukuzi wa umma, kufika majengo ya Bunge jijini Nairobi.
Wabunge walipoalikwa ikulu, alipewa lifti na mbunge mwenzake.
Hata hivyo, wakati wa kuondoka, alitumia gari la uchukuzi wa umma maarufu kama matatu.
„Nimetimiza ahadi yangu kwa mbunge kijana wa Igembe Kusini John Paul
Mwirigi katika ikulu ndogo ya Sagana," umesema ujumbe kwenye ukurasa wa
Facebook wa Rais Kenyatta.
Picha za mbunge huyo akikabidhiwa gari hilo zimepakiwa kwenye ukurasa huo wa Rais.
John Paul Mwirigi ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu Somo la Ualimu
katika Chuo Kikuu cha Mt Kenya alitangazwa mshindi baada ya kupata kura
18,867 na kumshinda mpinzani wake wa karibu Rufus Miriti wa chama cha
Jubilee chake Rais Kenyatta, ambaye alikuwa na kura 15,411.
Wagombea wengine, ambao wamekuwa wanasiasa kwa muda mrefu walikuwa ni
Mwenda Mzalendo aliyepata kura 7,695, Kubai Mutuma (6,331) na Raphael
Muriungi (2,278).
"Niliota nilikuwa nikitoa hoja katika bunge wakati nilikuwa kidato cha
tatu. Ndio wakati nilianza kuwauliza wanafunzi wenzangu kunifanyia
kampeni kwani ningehitaji kura zao mwaka 2017. Nimeshikilia nafasi za
uongozi shuleni na nyumbani," alisema Bwana Mwirigi.
Paul Mwirigi: Mbunge wa umri mdogo zaidi Kenya
Mwirigi alisema ajenda yake ya kwanza itakuwa kusaidia shughuli za biashara ya kilimo, kukuza ujasiriamali na kulea vipaji.
"Kwa kuwa mimi ninatoka kwenye familia maskini, ninaelewa maswala
yanayoathiri wakazi. Ajenda yangu muhimu itakuwa kubadilisha maisha ya
watu," anasema.
Chanzo-BBC