CLOUDS MEDIA GROUP YATANGAZWA KUWA MSHINDI WA TUZO YA DAUDI MWANGOSI MWAKA 2017



Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura akikabidhi tuzo Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 kwa Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon leo Jumamosi Septemba 16,2017 mkoani Tanga-Habari/Picha na Oscar Assenga na Kadama Malunde

Jopo la Majaji Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Uliotukuka ya Daudi Mwangosi mwaka limeitangaza Clouds Media Group kuwa mshindi wa Tuzo hiyo kwa mwaka 2017.

Tuzo hiyo imetolewa leo na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini UTPC wakati wa mkutano wake mkuu wa unaofanyika katika ukumbi wa Tanga Beach Resort mkoani Tanga.

Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa uongozi wa Clouds Media Group na Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura.

Mbali na kupewa tuzo hiyo,pia Clouds Media Group imekabidhiwa hati ya ushindi na hundi ya shilingi milioni 10 kama pole kwa changamoto waliyopitia baada ya kituo cha matangazo kuvamiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda aliyekuwa ameambatana na askari polisi.

Mwenyekiti wa Jopo la Majaji Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Uliotukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017,Jenerali Ulimwengu alisema madhumuni ya tuzo ya mwangosi ni kumuenzi na kumkumbuka kwa kumpa mwanahabari au chombo cha habari tuzo yenye jina lake.

“Jopo la majaji mwaka huu tunaitangaza Clouds Media Group kuwa mshindi wa tuzo ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 kwa sababu tarehe 17,Machi,2017 wanahabari wa Clouds walivamiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam akiwa na askari polisi akiwataka kutangaza habari ambayo hawakuitaka lakini wafanyakazi hao wakakataa kutangaza habari hiyo,huu ni ushujaa kwani hawakukubali kutii amri ambazo zilikuwa kinyume na kazi waliyofundishwa na uandishi wa habari”,alisema Ulimwengu.

“Lengo la tuzo hii iliyoanzishwa mwaka 2013 na UTPC ni kupinga vitendo viovu wanavyofanyiwa waandishi wa habari , hutolewa kwa mwandishi wa habari anayefanya kazi nchini aliyekutana na madhila katika utendaji kazi wake ama chombo cha habari ambacho kimekutana na madhila”,alieleza Ulimwengu.

Aliongeza kuwa tuzo hiyo inalenga kuwafanya wadau wa habari ikiwemo serikali kutambua kazi ya waandishi wa habari.

“Daudi Mwangosi alikuwa mwenyekiti Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Iringa,aliuawa Tarehe 2 mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo mkoani humo,akitekeleza majukumu yake,ni mwandishi wa habari wa kwanza nchini Tanzania kuuawa akiwa kazini, kifo chake kilishtua na kusikitisha watu wengi duniani”,alieleza.

Mshindi wa kwanza wa tuzo ya Daudi Mwangosi ni Absalom Kibanda.

Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura akikabidhi tuzo Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 kwa Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon

Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura cheti cha ushindi kwa Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon

Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura akikabidhi hundi ya shilingi milioni 10 kwa Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon.

Mwenyekiti wa Jopo la Majaji Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Uliotukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017,Jenerali Ulimwengu akizungumza wakati wa kutangaza mshindi wa tuzo hiyo mwaka huu.

Mkurugenzi wa UTPC Abubakar Karsan akielezea kuhusu Tuzo ya Daudi Mwangosi




Wajumbe wa mkutano mkuu wakiwa ukumbini

Meza kuu

Mkutano unaendelea

Rais wa UTPC Deogratius Nsokolo akizungumza ukumbini

Mkurugenzi wa UTPC,Abubakar Karsan,Mshindi wa kwanza wa tuzo ya Daudi Mwangosi,Absalom Kibanda na Mwenyekiti wa Jopo la Majaji Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Uliotukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017,Jenerali Ulimwengu wakiteta jambo.


 Habari/Picha na Oscar Assenga na Kadama Malunde
Powered by Blogger.