JENGO LA OFISI ZA MAWAKILI WA YUSUPH MANJI ZAVAMIWA NA WATU WASIOJULIKANA
Watu wanane wanaodaiwa kuwa ni wahalifu
wamevamia jengo la Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza na kufanya
uharibifu wa mali za wapangaji.
Jengo la Prime House lina ghorofa tano
lipo jirani na ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) wilayani Ilala jijini Dar es salaam.
Mwandishi ameshuhudia barabara ya
kuingia eneo hilo ikifungwa kwa muda na polisi ambao walitumia magari
yao kuziba njia na kuweka uzio wa utepe wa rangi ya njano.
Jengo la Prime House lina ofisi za
kampuni mbalimbali, zikiwemo za mawakili wa Yusuf Manji ambazo
zimevamiwa na wameondoka na nyaraka muhimu, duka la dawa na sehemu ya
kufanya mazoezi gym.
Mmoja wa mawakili ambao wana ofisi
katika jengo hilo, ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kwamba
watu hao walipofika walimfunga mlinzi kwa kamba na kisha kuingia ndani
kwa nguvu.
"Mlinzi ameniambia baada ya kuingia
walipokuwa wakifanya upekuzi walikuwa wakisikika wakisema si huku
tutazame ghorofa linalofuata si hili,” wakili huyo amemkariri mlinzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum
Hamduni amethibitisha tukio hilo akisema limetokea kati ya saa nane na
saa tisa usiku wa kuamkia leo.