RC MLINGWA, APIGA MARUFUKU KUVAA NGUO ZA VYAMA KWENYE MWENGE WA UHURU

MKUU wa mkoa wa Mara Charles Mlingwa amewataka wananchi kuacha kuvaa mavazi ya sare ya vyama vya siasa sambamba na hilo kuepuka kauli za kukashifu na kubeza mwenge wa uhuru unaoanza mbio zake hivi karibuni mkoani hapa.
Alisema hayo jana wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari juu ya ujio wa mwenge huo ambao ni sherehe inayothibitisha umoja wa kitaifa kwa sababu hiyo amewataka watu wavae mavazi ya kawaida ili kudumisha umoja huo kwa kuzingatia mwenge huo ndio ngao ya uhuru.
‘’Nasema hivyo kwasababu mamilioni ya watanzania wanafahamu thamani ya mwenge tunahamasisha umoja, na maendeleo kwa hiyo hao wachache wanawakera waliowengi wito wangu asiwepo mtu wa kuubeza mwenge wanaosema mwenge ni kibatari wanadharau nchi na kama akiwepo mtu wa aina hiyo atachukuliwa hatua za kisheria’’alisema.
Mlingwa alisema mkoa huo unatarajia kupokea mwenge huo agosti 23 mwaka huu katika eneo la Kisorya wilayani Bunda ukitokea mkoa wa Mwanza huku unatarajiwa kukimbizwa katika halmashauri za wilaya zipatazo tisa mkoani hapa mbio hizo zitamalizika septemba mosi mwaka huu.
Alisema mwenge huo utakimbizwa umbali wa kilomita 1054 ndani ya mkoa huo ukiwa umelenga jumla ya miradi ya shughuli za maendeleo 61 ambapo miradi 9 itawekewa mawe ya msingi miradi 17 kuzinduliwa, 16 kufunguliwa na miradi 12 kukaguliwa.
‘’Miradi hiyo itakuwa ni wilaya ya Bunda 9,Musoma miradi 10,Rorya miradi 7, Serengeti miradi 14, miradi hii ina thamani ya shilingi bilioni 11 zikiwemo nguvu za wananchi bilioni 4.7, michango ya halmashauri milioni 368.4, michango ya wahisani bilioni 2 na mchango wa serikali kuu bilioni 4’’alisema.
Alisema miradi hiyo iko katika sekta ya Kilimo, Afya, Viwanda, Maji, miundombinu, uvuvi, na maendeleo ya jamii huku ujumbe wa mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka huu ni ‘’Shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu’’ ujumbe unaozingatia vipaumbele na mikakati ya serikali ya awamu ya tano.
Alisema ujumbe wa mwaka huu umelenga kuelekea uchumi wa kati ambao misingi yake ni Tanzania ya viwanda ifikapo mwaka 2020 / 2025 kama dira ya maendeleo inavyoelekeza.