Mzee Aliyecharazwa VIBOKO Na Mkuu wa Wilaya Ashonwa Nyuzi 9
Chindika
Pingwa, mzazi aliyecharazwa viboko na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon
Odunga, amedai kushonwa nyuzi tisa kutokana na kipigo hicho.
Odunga
alimcharaza viboko Pingwa mwenye umri wa miaka 56 baada ya gari lake
kupigwa mawe na watoto wanne, wawili wakiwa ni wa mzazi huyo.
Tukio
hilo lilitokea Agosti 11 katika barabara ya Kondoa-Dodoma, kwenye
Kijiji cha Paranga wilayani Chemba ambapo gari la Mkuu wa Wilaya huyo
lenye namba za usajili STL 669 lilipigwa mawe na watoto na kusababisha
kioo cha nyuma kuvunjika.
Katika
mahojiano na mwandishi wa habari hii mwishoni mwa wiki iliyopita
wilayani Chemba, Chindika alisema amesikitishwa na kitendo kilichofanywa
dhidi yake na kiongozi huyo wa serikali.
Alisema hakuona sababu za kupigwa kwa makosa yaliyofanywa na watoto, ilhali tayari alikuwa mikononi mwa polisi.
Chindika
alisema kipigo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya huyo kimemsababishia majeraha
kwenye mkononi na kichwa ambapo alilazimika kushonwa nyuzi tisa.
"DC
(Mkuu wa Wilaya) alikuwa ananipiga kwa fimbo kubwa. Baadhi ya maeneo ya
mwili hasa mikononi yamevimba kutokana na kipigo, wakati ananipiga
nilikuwa najaribu kujizuia," alisema.
Alisema zaidi: "Mkuu
wa wilaya amenisababishia maumivu makali na alikuwa akinipiga huku
nikiwa nimefungwa pingu tayari kupelekwa katika kituo cha polisi Chemba
(kipo jirani na Kitongoji cha Morongia, Kijiji cha Kambianyasa).
"Kosa
lilifanywa na mtoto mdogo ambaye naye alikimbia, lakini pia wenzake
aliokuwa nao walikamatwa na kupigwa, ili waseme mwenzao aliyefanya kosa
hilo amejificha wapi."
Chindika
aliiomba serikali kuwapa onyo viongozi wanaojichukulia sheria mikononi
kupiga raia wasiokuwa na hatia, ili kuepuka kujenga uadui kati yao na
wananchi wanaowaongoza.
"Serikali
pia, iliangalie suala hili kwa kina kwa sababu linaweza kusababisha
maafa kwa wanakijiji na raia wasio na makosa kutokana na baadhi ya
viongozi kujichukulia sheria mkononi," alisema zaidi Pingwa.
"Mimi sielewi kitu gani kinaendelea dhidi ya kiongozi huyu wa serikali."
Mwenyekiti
wa Kitongoji cha Morongia, Marius Roman, akizungumza kuhusu tukio hilo,
alisema amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na Mkuu wa Wilaya huyo.
Alisema
masikitiko yake yanatokana na ukweli kuwa hakukuwa na sababu ya
kiongozi huyo kumpiga Pingwa, ilhali hatua za kisheria dhidi yake
zilikuwa zimeshaanza kuchukulia kwa kufungwa pingu na kuingizwa kwenye
gari la polisi.
"Kitendo hiki hakijawafurahisha wakazi wa eneo hili," alisema Roman. "Huu ni udhalilishaji na uonevu dhidi ya wananchi."
Mwenyekiti
huyo alisema kuna haja ya mkuu wa wilaya huyo, kwenda katika kitongoji
hicho na kuomba radhi wakazi wa eneo hilo kwa kitendo alichofanya.
"Licha
ya ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Chemba kusaidia kulipa gharama
za matibabu na usafishaji wa vidonda vya Chindika, bado haitoshi," alisema mwenyekiti huyo.
"Kinachopaswa ni mkuu huyo, kurejea kuongea na wananchi wa eneo hili na kuomba radhi."