Mkuu wa Wilaya Aamuru Mwalimu Akamatwe Baada ya Kushindwa Kutaja Jina Lake
Mkuu
wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa (pichani) anadaiwa kumweka mahabusu
mwalimu mmoja kwa kushindwa kutaja jina la kiongozi huyo.
Tukio
hilo lilianza kusambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii jana
ikielezwa kuwa mkuu huyo wa wilaya alimtaka mwalimu huyo achague kupiga
‘pushup’ 20 au polisi wakamkamate na kumsweka mahabusu.
Kutokana
na tukio hilo, Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimemjia juu mkuu huyo
wa wilaya kikidai kuwa maswali aliyokuwa akiyauliza mteule huyo wa Rais
John Magufuli hayakustahili na wala hayakuwa ya kitaaluma.
CWT
ilisema katika ziara hiyo ambayo mkuu wa wilaya alitembelea shule
mbili, aliwataka walimu wataje jina lake (la DC), shule imeshika nafasi
ya ngapi kitaifa na wataje majina ya magazeti ya Serikali.
Pia,
inadaiwa katika maswali yake hayo, mkuu huyo wa wilaya alimtaka mwalimu
huyo ataje tofauti ya CUF (chama cha siasa) na CAF ambalo ni Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika.
Mkuu
huyo wa wilaya alipopigiwa simu jana asubuhi ili azungumzie tuhuma
hizo, alisema yuko kwenye kikao na kuomba apigiwe simu baadaye.
Alipopigiwa
simu mara ya pili mchana alijibu: “Siwezi kuzungumzia suala hilo, nipo
kwenye kikao na walimu tangu asubuhi waandishi wananipigia simu
nawaambia hawanielewi.”
Hata
hivyo, jioni alipopigiwa tena kwa mara ya tatu na kuulizwa tena sababu
za kumuweka mahabusu mwalimu huyo alijibu: “Sikumuweka ndani mwalimu
huyo kwa sababu ya kushindwa kutaja jina langu, isipokuwa ni kwa sababu
ya kunikosea nidhamu.”
Jana,
mwalimu huyo wa Shule ya Sekondari Lerai, Erasto Mhagama alisema
aliwekwa mahabusu wiki iliyopita kuanzia saa 8:30 mchana hadi saa 2:00
usiku alipoachiwa huru.
Kwa
mujibu wa mwalimu huyo, polisi walimweleza kuwa amewekwa mahabusu kwa
amri ya mkuu wa wilaya bila kupewa sababu za kutendewa hivyo.
Mwalimu
huyo alisema kabla ya kukamatwa kwake, DC Byakanwa alifanya kikao na
walimu na alianza kwa kuwauliza wangapi wanamfahamu kwa majina yake,
lakini wote walikaa kimya.
Baada
ya kimya hicho, mkuu huyo wa wilaya aliwapa karatasi walimu wote ili
waandike majina yake, lakini wote walishindwa kuliandika.
Alisema
baada ya muda, mkuu huyo wa wilaya aliwataka waandike nafasi iliyoshika
shule hiyo kwenye Mtihani wa Taifa kwa mwaka 2015, mwalimu mmoja
inadaiwa alishindwa kuandika.
Mwalimu
huyo alifafanua kuwa mkuu huyo wa wilaya alimfuata yeye na kumtaka
aeleze Halmashauri ya Wilaya ya Hai ina shule ngapi, alimjibu kuwa
asingeweza kutaja kwa kuwa hakuwa na takwimu sahihi.
Alisema
majibu hayo yalimfanya kiongozi huyo apige simu polisi na kuwaagiza
wafike shuleni hapo haraka, lakini kabla hawajafika, alimwita pembeni na
kumtaka achague adhabu moja kati ya kwenda mahabusu au kupiga
‘push-up’.
“Aliniambia
nichague kupiga push-up 20 au niende mahabusu nilimwambia siwezi kupiga
push-up kwa sababu nina matatizo ya kiafya. Nikachukuliwa nikapelekwa
polisi Bomang’ombe,”alisimulia mwalimu huyo.
Mwenyekiti
wa CWT mkoani Kilimanjaro, Omary Mchome alisema kitendo kilichofanywa
na mkuu huyo wa wilaya hakikubaliki na ni kinyume cha maadili ya
kitaaluma na ya utumishi wa umma.
“Hiki
ni kitendo cha udhalilishaji, CWT hatutavumilia tutatoa tamko kali.
Kumweka mtu ndani kwa sababu ameshindwa kujibu maswali ni kudhalilisha
taaluma ya ualimu,” alisema Mchome.
Mwenyekiti
huyo alisema baada ya kupata taarifa hizo, viongozi walikwenda kwenye
shule mbili ambazo mkuu huyo wa wilaya alizitembelea wakapatiwa taarifa
ya kadhia hiyo.
“Baada
ya kupata taarifa nilimtuma Katibu wa CWT Mkoa wa Kilimanjaro na wa
Wilaya ya Hai kufanya mahojiano na walimu waliokuwapo katika kikao
hicho, walisema waliulizwa maswali ambayo si ya kitaaluma.
“Eti
unamuuliza mwalimu taja jina langu, shule yako imeshika nafasi ya ngapi
kitaifa, taja magazeti ya Serikali. Haya mambo yanaingiaje katika
taaluma? Na kama mtu huyafahamu ni kosa?” alihoji Mchome.
Mwenyekiti
huyo alisema katu hawatafumbia macho suala hilo kwakuwa ushahidi wanao
na jana au leo walitarajia kupeleka barua rasmi ya malalamiko kwa Mkuu
wa Mkoa Kilimanjaro.
Credit: Mwananchi