RAIS MAGUFULI AWACHANA WATUMISHI WA UMMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli leo wakati
akizindua Mfumo wa serikali wa ukusanyaji kodi kwa njia ya Kieletroniki
amewachana baadhi ya watumishi wake akisema wamekuwa wakiwaza mambo
makubwa ambayo wanashindwa hata kuyatimiza.
Rais Magufuli amesema kuwa watumishi wengi wamekuwa si wabunifu katika
kuangalia vyazo vya mapato ambavyo vinaweza kusaidia serikali kuingiza
pesa nyingi lakini wao wamekuwa wakiwaza kuongeza bei ya pombe tu na
kuacha vitu vingine ambavyo vingeweza kuongeza mapato kwa serikali kwa
njia nyingine nzuri.
"Saizi watu wanahangaika na Machinga wakati tungeweza kutengeneza
vitambulisho vya wamachinga na kila kimoja tukauza labda elfu kumi,
Machinga akinunua kitambulisho hicho anatambulika na serikali na
kinaeleza kuwa anapaswa kuwa wapi, je, ni shilingi ngapi tungezipata
hapo kwa idadi wa wamachinga waliopo nchi nzima? Lakini watu wetu wao
wanawaza kuongeza bei ya pombe tu, yaani tuna watu wa uchumi wengi
lakini sijui hata wanafikiria nini " alisema Rais Magufuli
Mbali na hilo Rais Magufuli alisema hata tabia ya watu kukwepa kulipa
kodi inasababishwa na mipango mibovu akitolea mfano kuwekwa bei juu ya
kodi ya majengo jambo ambalo linafanya watu wengine kushindwa kulipa
kodi hiyo na serikali kupoteza mapato.
"Watu wetu hawa hata kwenye kodi ya majengo unakuta wameweka mtu alipe
milioni mbili sasa hizo pesa wananchi wanazipata wapi? Ndiyo maana
wanakwepa kodi sababu hawana pesa hizo lakini kama wangeweka labda elfu
kumi, ishirini mpaka hamsini halafu wenye maghorofa labda laki mbili
ungeona kila mtu angekimbilia yeye mwenyewe kulipa kodi, kwa nyumba zote
zilizopo Tanzania tungepata shilingi ngapi? Lakini wameweka pesa kubwa
na hawazipati sababu watu hawalipi hawana hizo pesa" alisisitiza Rais
Magufuli
Katika hatua ya mwisho Rais Magufuli aliyaomba makampuni ya simu nchini
yawe mfano wa kuigwa na ikiwezekana yawe ya kwanza kabisa kujiunga
katika mfumo huu mpya wa ukusanyaji wa kodi kwa njia ya kieletroniki
kwani mfumo huu una manufaa kwa wawekezaji na Watanzania kwa ujumla.