MBUGA ZA WANYAMA UNAZOWEZA KUTEMBELEA BURE WIKENDI HII
Siku ya Jumatatu ya Juni 5 itakuwa ni
maadhimisho ya ‘Siku ya Mazingira Duniani’ ambayo huadhimishwa na
mataifa tofauti duniani ikiwa imebeba kauli mbiu ya ‘Kuwaunganisha Watu
na Mazingira Asilia.’
Mapema wiki hii Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mh. January
Makamba alitoa taarifa kwa umma kuwa kwa hapa nchini maadhimisho ya
siku hiyo kitaifa yatafanyika kijijini Butiama mkoani Mara, mahali
alipozaliwa mwasisi wa taifa la Tanzania, Hayati Mwl. Julius Nyerere,
ikiwa ni kuenzi jitihada zake za kulinda na kuhifadhi mazingira.
Katika kunogesha sherehe hizo Waziri
huyo amesema kuwa serikali imetoa ofa kwa wananchi kutembelea hifadhi
yoyote ya mbuga ya wanyama bila ya kiingilio chochote kwa siku tatu,
kuanzia Ijumaa ya Juni 2 mpaka Jumapili ya Juni 4. Alisema kuwa lengo
kubwa ni kuona uwepo wa wanyama na kujifunza kuwa mazingira yanahitaji
kulindwa zaidi na zaidi.
Kauli hiyo ya Waziri imekuja siku chache
baada ya kampuni inayojihusisha na masuala ya huduma za hoteli
mtandaoni barani Afrika, Jumia Travel kuzindua kampeni ya
‘DemocratizeTravel’ inayolenga kuwakomboa waafrika na watanzania
kiujumla katika kusafiri na kutalii vivutio mbalimbali nchini huku wao
wakirahisisha huduma za malazi na hoteli.
Kampuni hiyo inalenga kuhamasisha na
kutoa elimu juu ya dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa wananchi ya
kwamba mchakato mzima unaohusisha utalii ni gharama. Katika
kulifanikisha hilo kampuni hiyo imedhamiria kuelimisha juu ya vivutio
vilivyopo nchini, masuala ya msingi ya kuzingatia wakati wa kusafiri
pamoja na kurahisisha gharama za malazi kupitia hoteli za kila hadhi
zilizopo kwenye mtandao wao wa travel.jumia.com.
Baadhi ya changamoto zilizopo ni pamoja
na mwamko mdogo wa watanzania kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo
karibu na wanayoishi. Wapo baadhi yao hawafahamu kuwa wanaishi na
vivutio hivyo na wengine huchukulia mchakato mzima unahusisha gharama
kubwa.
Vifuatavyo ni baadhi ya vivutio vya
kitalii ambavyo watanzania mahali popote walipo wanaweza kwenda
kuvitembelea wikendi hii bure kabisa kwa mujibu wa kauli ya serikali
katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.
Kanda ya Kaskazini. Mikoa ya
Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Mara kwa kiasi kikubwa imebarikiwa kuwa
na hali ya hewa nzuri inayowavutia watalii, hifadhi za mbuga za wanyama,
maeneo yenye masalia ya kale pamoja na milima ya kuvutia. Vivutio
vinavyopatikana huko ni kama vile; Hifadhi za Taifa za Arusha, Mkomazi,
Ziwa Manyara, Mlima Kilimanjaro, Serengeti na Ngorongoro.
Kanda ya Magharibi. Eneo hili
inapatikana mikoa kama vile ya Kigoma na Rukwa ambayo nayo haijaachwa
nyuma kwa upande wa vivutio vya kitalii. Wananchi wanaoishi katika au
karibu na mikoa hii wanaweza kutembelea Hifadhi za Mbuga za Wanyama kama
vile; Gombe, Katavi, Mahale, Rubondo na Saanane na kujionea wanyama
wengi hususani sokwe wa kipekee.
Kanda ya Kusini. Morogoro,
Iringa, Mbeya na Ruvuma ni baadhi ya mikoa inayoweza kupatikana katika
ukanda huu ambapo kuna hifadhi za kitaifa kama vile; Kitulo, Mikumi,
Ruaha na Udzungwa. Mbuga kama vile Mikumi inajulikana kuwa na idadi
kubwa ya wanyama kama vile pundamilia, nyati na tembo.
Kanda ya Mashariki. Ukanda huu
kwa kiasi kikubwa umepakana na fukwe ya bahari ya Hindi ambayo
inapatikana kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na
Mtwara. Mbali na kuwa na hoteli nyingi zilizojengwa pembezoni mwa fukwe
ya bahari hiyo lakini pia mikoa hiyo inavyovivutio vingine lukuki kama
vile; Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Mji wa Bagamoyo, Kisiwa cha Kilwa,
Mapango ya Amboni na Mikindani.
Visiwa vya Zanzibar. Hakuna
anayeweza kubisha kuwa vivutio mbalimbali vilivyomo visiwani humo
hususani fukwe nyingi safi na za kuvutia pamoja na hoteli za kifahari
ndivyo huwatoa watu kutoka mataifa mbalimbali duniani kwenda kuzuru.
Mbali na visiwa hivi kusifika kuwa na sehemu nzuri za kupumzika bali pia
vina utajiri mkubwa wa tamaduni za watu wa mataifa mbalimbali waliopata
kuishi humo kama vile Waarabu, Waingereza pamoja na waafrika kwa
ujumla. Lakini pia kuna majengo ya kale yaliyojengwa karne nyingi
zilizopita ambayo mpaka leo hii bado yapo na vinginevyo vingi.
Uzuri wa nchi ya Tanzania umebarikiwa
kuwa na vivutio vya kila namna karibuni kila mkoa. Hivyo kisingizio cha
kutotembelea sehemu fulani kwa sababu ipo mbali kinakuwa hakina mantiki,
Jumia Travel inakushauri anza kwanza na vilivyo karibu nawe na fursa
hii iliyotolewa na serikali inaweza kuwa ni mwanzo mzuri kwako.
Na Jumia Travel Tanzania