RAIS MAGUFULI AKUTANA NA MAKAMANDA WA POLISI TANZANIA,AWAPA MAAGIZO
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amelitaka Jeshi la Polisi nchini kutumia weledi wake kwa kiwango cha juu
katika kutekeleza jukumu lake lakulinda raia na mali zao, hasa
kukomesha vitendo vya uhalifu.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 02 Juni, 2017 wakati
akizungumza na Makamanda Wakuu kutoka makao makuu ya polisi, Makamanda
wa Mikoa na Vikosi vya Tanzania Bara na Zanzibar na viongozi wote wakuu
wa polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam waliokutanakatika Bwalo la Maofisa
Wakuu wa polisi lililopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Dkt. Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa juhudi zake za
kukabiliana na uhalifu lakini ametaka juhudi hizo ziongezwe
hususanikukabiliana na matukio ya ujambazi na mauaji ya raia, dawa za
kulevya na kuendesha operesheni zenye tija katika mikoa yote.
Amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro kujipanga
vizuri yeye na safu yake ya Makamanda, Viongozi Wakuu wa Vikosi na
Maofisa mbalimbali ili kuondoa dosari zote za utendaji kazi zinazoshusha
ufanisi na heshima ya Jeshi la Polisi.
“Ni lazima ufanye mabadiliko makubwa, nataka kuona Jeshi la Polisi
linakuwa Jeshi la Polisi, Wewe IGP Sirro na Makamnda wenzako hakikisheni
mnakomesha uhalifu, komesheni mauaji dhidi ya raia, ujambazi na dawa za
kulevya” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Makamanda, Maofisana Askari wa jeshi
hilo kujiepusha na rushwa, dawa za kulevya, kutumiwa na watu kwa maslai
binafsi, kuingia mikataba isiyo na maslai kwa Jeshi na Taifa,
ubadhirifu na kuacha upendeleo katika utoaji wa ajira na vyeo.
Mhe. Rais Magufuli pia ametaka Makamanda, Maofisa na Askari wote wa
Jeshi la Polisi wampe ushirikiano wa kutosha IGP Simon Sirro ambaye hivi
karibuni amemteua kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.
Mwigulu Lameck Nchemba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi Meja Jenerali Mstaafu Projest Rwegasira.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Juni, 2017