RAIS MAGUFULI AAGIZA KAMPUNI ZA SIMU ZIFUTWE
Rais
John Magufuli ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuta
kampuni za simu za mkononi zote ambazo hazitaki kujiandikisha katika
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Aidha,
amezitaka kampuni mbalimbali kujisajili katika mfumo wa ukusanyaji kodi
za serikali kwa njia ya kielektroniki, aliouzindua jijini Dar es Salaam
jana, mfumo unaosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) na Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA).
“Tulipitisha
sheria kwamba makampuni ya simu yote lazima yasajiliwe kwenye soko la
hisa la Dar es Salaam, wamesuasua weee, wamezunguka …TCRA msitoze faini,
futeni hizo kampuni,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa faini ambayo imewekwa na TCRA ni ndogo, hivyo kampuni hizo haziogopi.
Alisema
kituo hicho kilichoanza kazi Oktoba mwaka jana, mwitikio wa kujiunga
sio mkubwa, ambapo ni kampuni tatu pekee ambazo zimejiunga na alihimiza
zingine kujiunga.
Rais
Magufuli alisema kwa kutumia kituo hicho, makusanyo ya kodi hayatakuwa
na malalamiko tofauti na huko awali kulikuwa na malalamiko kwa wakusanya
kodi na pia walipa kodi wakidai kuongezewa viwango.
“Tulikuwa
tukitumia makusanyo ya kodi ya mtu na mtu na huyo mtu inategemea
uaminifu wake, wapo ambao sio waaminifu wanapokwenda kwa wateja
wanawakadiria makadirio ya juu na pia walipakodi kudanganya
wanachopata,” alisema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli alisema mwarobaini wa malalamiko hayo ni mfumo huo, ambao ni
mashine zinakokotoa na kwamba hakuna mwingilio wa mtu katika hesabu.
“Wengine wote ambao hamjajiunga mfanye hivyo kwa hiari, mlipa kodi na mkusanya kodi mnatakiwa kuishi kwa raha na upendo,” alisema
Rais Magufuli na kuongeza kuwa kama wafanyabiashara hao wanataka mpaka
sheria ibadilishwe ndipo watii agizo hilo, serikali inaweza kupeleka
muswada kwa hati ya dharura.
“Najua
mnaweza kufafuta visababu kama mnataka mpaka tubadilishe sheria bado
Bunge linaendelea kule, tunaweza kufanya mabadiliko,”alisema na
kuziomba kampuni hizo kushirikiana na serikali, isionekane kwamba
serikali haitaki kushirikiana na wawekezaji kwa kuanzisha mfumo huu.
Aidha,
alisema serikali hii inawapenda wawekezaji ndio maana inawawekea
mazingira bora ya biashara sambamba na ukusanyaji kodi ulio sahihi.
“Niwaombe
ndugu zangu, na hii nawaomba kutoka moyoni mwangu tunahitaji kodi, nchi
zote zinalipa kodi, ni lazima kila mmoja alipe kodi awe anataka au
hataki,” alisema.
Rais
Magufuli aliziomba kampuni za simu pamoja na kampuni nyingine, kuingia
katika mfumo huo ili kuwe na usawa katika ukusanyaji wa kodi.
Alisema
anachukia wawekezaji pamoja na ubinafsishaji wa mali za umma wa hovyo,
ambao hauna faida kwa nchi ambapo alisema kuna zaidi ya kampuni 197
zimekufa.
“Naeleza
yote haya ili muelewe serikali ninayoiongoza inataka nini, inataka
kufanya biashara na wawekezaji ambao ni waaminifu, biashara yoyote
lazima iwanufaishe na wenye nchi,” alisema.
Aidha,
Rais Magufuli alizitaka wizara zote zisimamie kampuni kuingia katika
mfumo huo, ambao utawasaidia pia katika biashara zao kujua mapato yao.
“Hakuna
mtu duniani anayependa kulipa kodi, hata enzi za Yesu, na walipa kodi
katika enzi zote hawakupendwa, usitegemee wewe kamishna TRA, ZRA
utapendwa, wewe kusanya tu,” alisema Rais Magufuli.
Alisema
nchi inapoteza fedha nyingi kupitia mianya ya upotevu wa mapato, lakini
serikali iliamua kujenga kituo hicho kwa lengo la kuhakikisha na
kulinda usalama wa taifa na taasisi za serikali na kampuni binafsi
pamoja na kuimarisha na kukuza sekta ya teknolojia ya habari na
mawasiliano.
“Kampuni
ambazo zitatunza taarifa zao kwenye kituo hiki zitakuwa na uhakika wa
usalama wa taarifa zao hata kama uharibifu wowote utatokea,” alisema.