BINTI ACHOMA MOTO NYUMBA AKIMKOMESHA MPENZI WAKE HUKO SINGIDA

Jeshi la polisi mkoani Singida,linamshikilia mkulima mkazi wa Mitunduruni mjini hapa, Mariamu Juma (21), kwa tuhuma ya kuchoma nyumba moto na kuteketea pamoja na mali zote zilizokuwemo.
Kwa mujibu wa kamanda Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Debora Magiligimba, kitendo hicho kimechangiwa na wivu wa kimapenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda Magiligimba,alisema kuwa tukio hilo limetokea Mei 30 mwaka huu saa 11.40 jioni, huko maeneo ya Mwenge tarafa ya Mungumaji Manispaa ya Singida.
Akifafanua, alisema kuwa siku ya tukio mtuhumiwa alienda kwenye nyumba aliyopanga mpenzi yake Benardo Mabula, ambayo inamilikiwa na Omari Hamisi (35) katika maeneo ya Mwenge mjini hapa.
“Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo, ni wivu wa kimapenzi. Mtuhumiwa Mariamu alipoingia kwenye chumba cha rafiki yake wa kiume (Mabula),aliwasha moto kwa kiberiti kwa lengo la kuchoma vifaa vya mpenzi wake,” alisema na kuongeza;
“Lakini moto huo ulisambaa vyumba vyote vya nyumba hiyo na kuteketeza kila kitu.Hadi sasa thamani ya nyumba na mali iliyoteketea, bado haijafahamika.”
Kamanda huyo alisema kuwa baada ya uchunguzi kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili. Mpenzi wa mtuhumiwa Mariamu,amefanikiwa kutoroka na kukimbilia kusikojulikana.
“Jeshi la Polisi mkoani hapa,linatoa wito kwa wananchi wote hasa familia zenye migogoro ya ndoa,wafike ofisi zetu za dawati la jinsia na watoto zilizopo kila wilaya, ustawi wa jamii na viongozi wa dini, ili waweze kusikilizwa matatizo yao, badala ya kujichukulia sheria mkononi,” alisema Magiligimba.
Katika hatua nyingine, Kamanda huyo alisema vikongwe wawili wamefariki dunia papo hapo, baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba iliyojengwa kwa tofali za tope na kuezekwa kwa bati.
Magiligimba alisema vikongwe hao na watu wengine, walikuwa kwenye nyumba hiyo, kushiriki mazishi ya Mwajuma Mwendo aliyefariki Mei, 28 na kuzikwa kesho yake.
Aliwataja vikongwe hao kuwa ni Nzitu Mkumbo (80) mkulima kwa kijiji cha Mwangeza ambaye alivunjika miguu yote na mkono wa kushoto.Mwingine ni Kimwana Kingu (90) mkulima wa kijiji cha Mazangila, ambaye alivunjika mguu wa kulia na kujeruhiwa vibaya mguu wa kushoto. Vijiji hivyo vipo wilaya ya Mkalama.
Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Fatma Alli (70), Zena Ntoga (40), Kimwana Mohammed (70), Gyoli Kingu (45), Habiba Hussein (40) na Sophia Mashimba (50).
Alisema chanzo cha tukio hilo ni uchakavu wa nyumba hiyo iliyoanguka baada kupigwa na upepo mkali na kusababisha ukuta wa ndani uliotenganisha chumba na sebule, kuanguka.
“Jeshi la polisi mkoa wa Singida,linatoa wito kwa wananchi wote wawe na utaratibu wa kukarabati nyumba zao mara kwa mara.Pia tunawashauri wapande miti kwa wingi kuzunguka maeneo ya makazi yao,” alisema kamanda Magiligimba.
Powered by Blogger.