WAZIRI MKUU ATULIZA MJADALA WA MCHANGA WA MADINI BUNGENI
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wawekezaji wa madini nchini
kuondoa hofu ya kukosa haki zao kwani kamati ya pili iliyoagizwa kufanya
uchunguzi kuhusu mchanga wa madini (makinikia) bado haijakamilisha kazi
yake.
Waziri Mkuu alisema hayo jana wakati akijibu swali la mbunge wa Tabora
Mjini, Emmanuel Mwakasaka, lililohoji kuhusu taswira ya Tanzania
kimataifa hasa katika uwekezaji wa madini.
Majaliwa aliwataka wawekezaji wa madini kuondoa hofu kwa kuwa kamati ya
pili iliyoundwa kuangalia athari za kisheria, kisiasa na kimataifa
kuhusu sakata la mchanga wa madini bado haijatoa ripoti yake.
“Watanzania wengi walikuwa na hofu, hata wabunge wengi katika serikali
hii ya awamu ya tano mmekuwa mkizungumzia sakata la mchanga wa madini,
lakini niwatoe hofu, Rais John Magufuli alifanya hayo kwa nia njema ya
kulinda rasilimali za Taifa,” amliema
Waziri Mkuu aliwataka wawekezaji wa madini kuondoa hofu kwa kuwa
serikali itazingatia ushauri kutoka sekta nyingine kabla ya kuchukua
hatua katika sakata hilo la mchanga wa madini.