Baadhi ya
wanufaika wa TASAF III wa Kijiji cha Migato wakiimba wimbo maalum wa
kuwakaribisha wataalam kutoka TASAF Makao Makuu, Benki ya Dunia na wadau
wengine wa maendeleo (wadau washiriki wa mradi) ambao ni UNDP, UNFPA, ILO na
Umoja wa Nchi za Ulaya(EU) waliofika kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi
wa TASAF III Wilayani Itilima mkoani Simiyu
Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
umesikitishwa na kitendo cha wanufaika kutotimiza masharti ya mpango huo hali
inayosababisha kukosa fedha katika ruzuku hiyo kwa kaya maskini.
Hayo yalibainishwa jana na
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa ndani kutoka makao makuu (TASAF) Christopher
Sanga alipotembelea wanufaika katika kijiji cha Migato wilayani Itilima mkoani
Simiyu na kusema kuwa lengo la serikali kuwanufaisha ni kuwakwamua kimaisha.
Alisema kuwa serikali inatoa fedha
hizo kupitia ruzuku ya masharti ili watoto waweze kupata mahitaji yao ya kila
siku ikiwemo huduma ya elimu na matibabu kwa kupelekwa kliniki.
Sanga aliwataka wazazi kuwapa nafasi
ya kwenda shule watoto ili kutimiza masharti ya mpango huo ana pia waweze
kufikia malengo ya serikali ya kunusuru familia zao.
‘’mnaonekana kurudisha nyuma
jitihada za serikali ambazo lengo lake ni kuwaondoa katika hali mliyokuwa nayo
awali ya umasikini na kupiga hatua kimaisha katika kukidhi mahitajia ya kila
siku’’ alisema Sanga.
Aliongeza kuwa changamoto ya
kutotimiza masharti kwa wanufaika hao bado ni tatizo hali inayosababisha kaya
kupoteza ruzuku yake na kupungua kwa malipo ya wanufaika.
Alisema kuwa Lengo la serikali ni
kujenga nguvukazi ya watu wake katika kutatua kero za wananchi na mtoto
asipopelekwa kliniki akiwa mdogo, uzalishaji utapungua akiwa mkubwa.
Nao baadhi ya wanufaika wa mpango
huo walikiri kuwepo kwa baadhi ya familia kutotimiza masharti ya ruzuku hizo na
kusababisha fedha kurudishwa TASAF makao makuu.
‘’kuna baadhi ya familia watoto
hawafiki shuleni, lakini asubuhi wanaaga na kuvaa sare kwenda shule…hivyo ni
jukumu la kila mzazi kuhakikisha mtoto wake anahudhuria masomo ili aweze
kutimiza masharti ya mpango huu’’ alisema Minza Bulayi Mkazi wa Migato.
Katika kipindi cha mwezi Novemba
hadi Disemba kaya 29 kati ya 99 kijijini hapo hazikuchukua ruzuku kutokana na
sababu mbalimbali ikiwemo walengwa kushindwa kutimiza masharti ya Elimu na Afya
kwa lengo la kuwa na jamii yenye afya na elimu bora kwa watoto.
|