POLISI YA ROBOTI YAZINDULIWA DUBAI KULINDA WATU DHIDI YA UHALIFU
Polisi nchini Dubai wamezindua afisa roboti ya kwanza itakayo piga doria
katika majumba ya kibiashara na maeneo ya kivutio kwa watalii.
Watu wataweza kuripoti uhalifu, kulipa faini na kupata taarifa kwa kugusa kompyuta iliopo kifuani mwa roboti hiyo.
Taarifa inayokusanywa na roboti hiyo itasambazwa kwa maafisa wa usafiri na trafiki.
Serikali inasema inalenga kuwa 25% ya kikosi chake kiwe ni cha roboti
kufikia 2030 lakini roboti hizo haziwezi kuichukua nafasi ya binaadamu.
"Nafasi za maafisa wa polisi hazitochukuliwa na mashine hii," amesema
Brigedia Khalid Al Razooqi, mkurugenzi mkuu wa huduma za kisasa
kielektroniki katika idara ya polisi Dubai.
"Lakini kutokana na kuongezeka idadi ya watu Dubai tunataka tuwahamishe
maafisa wa polisi ili wafanye kazi katika maeno yanayostahili na waweze
kushughulikia kikamilifu kuimarisha usalama mjini".