KIVUKO KIPYA CHA 'MV KAZI' CHAFANYIWA MAJARIBIO DAR ES SALAAM
Hatimaye kivuko kipya cha MV KAZI
kimefanyiwa majaribio ya kubeba abiria na magari kwa mara ya kwanza
Jijini Dar es Salaam baada ya kukamilika kwa matengenezo yake.
Majaribio hayo yalifanyika kulingana na
sheria na taratibu za vyombo vya majini ambayo inavitaka vyombo vyote
vya majini kufanyiwa majaribio kabla ya kuanza kazi ili viweze kupatiwa
cheti cha ubora “Seaworthiness Certificate”.
Awali wataalam kutoka Chuo cha Ubaharia
Dar es Salaam (DMI) waliweza kupima ubora na uimara wa kivuko hicho kwa
kutumia utaratibu wa kuweka mawe yenye kilo zinazolingana na uwezo wa
kivuko pamoja na magunia ya mchanga ili kuweza kupima uwezo wa kivuko
kulingana na mahitaji yaliyoainishwa kabla hakijabeba abiria na mizigo.
Zoezi hili pia lilihusu kufanyika kwa
kipimo cha kuhakikisha kuwa kivuko hakilali upande mmoja yaani
“Inclination test” ambapo kilionyesha Kivuko kiko sawa. Taarifa ya zoezi
hili itakuwa sehemu ya vitu vya makabidhiano wakati wa upokeaji wa
Kivuko.
Ujenzi wa MV KAZI umegharimu Shilingi
Bilioni 7.3 za Kitanzania na kina uwezo wa kubeba abiria 800 magari 22
sawa na jumla ya tani 170. Kivuko hicho kitakabidhiwa rasmi hivi
karibuni kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa ajili ya kuanza
kutoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni Jijini Dar es salaam na
kuongeza idadi ya vivuko katika eneo hilo kufikia vitatu.
Kivuko cha MV KAZI kikiondoka kwa mara
ya kwanza kutokea Magogoni kuelekea Kigamboni kikiwa na abiria na
magari. Kivuko hicho kilikua kikifanyiwa majaribio mara baada ya ujenzi
wake kukamilika kabla ya kukabidhiwa kwa TEMESA.
Abiria wakiingia katika kivuko cha MV
KAZI tayari kwa kuvuka kuelekea upande wa Kigamboni. Kivuko hicho
kilikua kikifanyiwa majaribio ya kubeba abiria kwa mara ya kwanza baada
ya ujenzi wake kukamilika hivi karibuni.