PAMOJA MAJAALIWA, ACHA IFIKE 2017-18 NIWAONE AKINA ABDULRAHMAN MUSA NA MBARA WA KAGERA



Na Saleh Ally
MSIMU wa Ligi Kuu umemalizika kwa Yanga kubeba ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kwa kuwa wamelingana pointi na watani wao wa jadi Simba.

Gumzo kubwa limeendelea kuwa ni nani hasa ni bingwa kwa kuwa Simba wamepeleka malalamiko yao kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), wakipinga Kagera Sugar kurejeshewa pointi tatu na mabao matatu ambazo wao walikuwa wamepewa kutokana na kubainika beki Mohamed Fakhi alicheza akiwa na kadi tatu za njano.

Hilo tunawea tukawaachia wao wakaendelea nalo kulijadili kadiri siku zinavyokwenda ziwe chache au nyingi, tutajua ambacho kimeendelea.

Ninachojadili na wewe msomaji ni vijana wawili wa Kitanzania, Abdulrahman Musa wa Ruvu Shooting na Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar ambao kwangu ndiyo nawaona ni mashujaa katika ufungaji wa mabao.

Hawa hawajaingia katika kuwania ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) ambao wametangaza wachezaji watano walioingia katika nafasi hiyo kuwa ni Simon Msuva, Haruna Niyonzima (Yanga), Aishi Manula (Azam FC), Shiza Kichuya na Mohamed Zimbwe (Simba).
,
Katika hali ya kawaida unaweza unapozungumzia msaada wa mchezaji, hakika unaweza pia na kuangalia uwezo wa timu. Mchezaji mmoja anayeweza kuibeba timu mwenyewe, akalingana na yule aliye katika timu yenye msaada mkubwa, unaweza kuangalia.

Kitu cha kwanza unapoangalia mchezaji bora, hakika lazima uanze na uwezo wake na msaada katika kikosi. Baada ya hapo, unaweza kuangalia masuala ya kadi ingawa kadi nazo unaweza kuangalia nafasi anayocheza.

Binafasi kutoingia kwa Mbaraka na Abdulrahman katika uchezaji bora naona si sawa na ninaweza kuiita ni uchaguzi wa mazoea. Sina sababu ya kulaumu ndiyo maana naweza kuelekeza maneno yangu mengi kwa wachezaji hao wawili.

Nimeipata ile habari ya bao la 14 la Abdulrahman ambaye amefikisha mabao 14 na kuwa sawa na Simon Msuva. Sasa wao ni wafungaji bora ingawa kama watatumia kigezo cha penalty, yeye atakuwa bora zaidi kwa kuwa Msuva kafunga penalti nne nay eye mbili tu.

Abdulrahman alikataa kufanyiwa mabadiliko, licha ya kutibiwa zaidi ya dakika 15, lakini alitaka kurejea uwanjani na aliamini angefunga. Kweli alirejea uwanjani akiwa na bandeji kichwa kizima, akafanikiwa kufunga bao lake la 14, zikiwa zimebaki dakika tano mpira kwisha.

Aina hiyo ya mpiganaji, inaonyesha Abdulrahman ni askari mwenye njaa ya mabao. Fowadi anayetaka kutimiza ndoto zake na hili ni jambo la kuvutiwa na inaonyesha wazi kuwa yeye na Mbaraka ni watu wanaotakiwa kupewa moyo wa kuendelea kufanya vizuri.
Mbarak alikuwa akiaminika ataifunga Simba ilipokutana na Kagera kule Bukoba, kweli alifanya hivyo. Wengi wakaamini atakuwa hatari kwa Yanga zitakapokutana Dar es Salaam, kweli alifanya hivyo. Na hizo ndiyo timu zenye safu ngumu ya ulinzi kwa mujibu wa takwimu.

Msimu huu ndiyo umepita na wenyewe wawili wameonyesha kweli wanaweza na wanastahili kupongezwa. Lakini najiuliza msimu ujao je? Vipi Abdulrahman na Mbaraka wa 2017-18 watakuwaje? Watakuwa hawahawa au ndiyo wale wachezaji wa msimu mmoja?

Wamepita wachezaji wengis ana wakifanya vizuri msimu mmoja na kuwa gumzo. Lakini wanapoingia msimu unaofuata huyeyuka kama upepo. Baada ya hapo utawasikia wakilaumu au kutosikika tena.

Nafikiri unajua tokea lini umeanza kuwasikia wachezaji kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakitamba. Huenda wanaweza kuwa mbali sana, lakini Kelvin Yondani au Juma Kaseja wanaweza kuwa funzo kwao. Kwamba wamefanya vizuri tokea linin a wao waendeleze wanachokifanya ili kufanya vizuri zaidi na baada ya hapo, kutakuwa na uamuzi sahihi katika mengi kuhusu wao.
Powered by Blogger.