UNAPOZUNGUMZIA BAYERN, ROBBEN, RIBERY NI SAWA NA WAFALME
Na Saleh Ally
HUU
ni mwaka wa 11 sasa tangu Mfaransa, Franck Henry Ribery alipojiunga na
kikosi cha Bayern Munich na huenda ameendelea kuwashangaza wengi
kutokana na mafanikio ambayo ameendelea kuyapata.
Ribery
sasa ana umri wa miaka 35 na amekuwa akiendelea kufanya vizuri akiwa
tegemeo la Bayern Munich ya Ujerumani kwa miaka yote 11.
Kwa sasa, tayari Bayern wameshabeba ubingwa wa Bundesliga ambayo kwa hapa nchini huonyeshwa kupitia ving’amuzi vya StarsTimes.
Lakini
Ribery ni kati ya wachezaji walioiongoza Bayern kufika nusu fainali ya
Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa pamoja na AS Roma, Liverpool na mabingwa
watetezi, Real Madrid.
Ribery
alianza kutamba mwaka wa kwanza tu tokea ametua Bayern akitokea
Marseille ya kwao Ufaransa na kukawa na mambo mengi kutokana na
yanayotokea.
Kwani
msimu wa kwanza tu alifanikiwa kufunga mabao 11 akiwa na asisti 8,
hivyo kumfanya baadaye kutangazwa mwanasoka bora wa Ujerumani.
Ukiona
sasa anaendelea kutamba Bayern unaweza kudhani maisha yake ni rahisi
lakini amekuzwa na fedha za kazi za vibarua alizokuwa akifanya baba yake
mzazi na wakati fulani aliingia kufanya kazi hizo hadi alipoona
anastahili kuendeleza ndoto yake katika soka.
Kupitia timu maarufu kama Metz, Galatasaray na sasa Bayern, kumbuka Ribery amekuwa mwanasoka bora wa Ulaya mwaka 2013.
Huyo
ni Ribery, lakini ana rafiki yake, Arjen Robben. Huyu ana miaka 34,
pungufu ya mmoja wa Ribery. Yeye alijiunga Bayern miaka miwili baadaye,
yaani 2009 akitokea Real Madrid.
Hadi
sasa tayari ana miaka tisa naye anaendelea kung’ara na kuwa shujaa.
Kipindi ambacho hatasikika, basi ni majeruhi lakini baada ya hapo lazima
atakuwa tegemeo kama iliyo kwa Ribery.
Robben
anatokea Uholanzi na maisha yake wakati akiwa mtoto hayakuwa mazuri
sana na baba yake aliishi akifanya kazi za kawaida tu na maisha yalikuwa
ni ya kuunga kiana.
Baada
ya kuanza kufanikiwa katika mpira, Robben aliamua baba yake mzazi awe
wakala wake na hadi sasa amekuwa akifanya kazi hiyo na kuendelea
kujiingizia kipato chake na anaendesha maisha yake.
Wawili
hawa wanafanana sana kutokea maisha ya awali lakini mwendo waliofikia
sasa na siri yao kubwa pamoja na kwamba wana vipaji ni kujituma bila ya
kuchoka na ile kuwa na ndoto ya kutaka kupata mafanikio.
Pamoja
na kwamba wanaonekana ni kama “wamezeeka” lakini wao ndiyo vyuma vya
Bayern. Siku wakiwa fiti wote na katika kiwango sahihi basi ujue kazi
inayofanyika katika “mabawa” ya Bayern kutoka kushoto na kulia, lazima
itamuumiza mpinzani.
Ukibahatika
kufika katika Jiji la Munich nchini Ujerumani, wawili hao hujulikana
kama pacha na kila mmoja ana sifa yake. Robben ni mpole, ila mjeuri.
Ribery ni mkimya ila mjeuri ile mbaya.
Kinachovutia
zaidi ni heshima kubwa wanayopata kutoka kwa Wajerumani ambao wanaamini
katika utendaji bora wa kazi kwa kujituma bila ya kuchoka na
kutobweteka baada ya kupata mafanikio.
Robben
amebeba ubingwa wa Bundesliga kwa misimu saba, ameshinda Kombe la
Ujerumani mara nne, akachukua Super Cup ya Ujerumani mara moja, Ligi ya
Mabingwa mara moja na Uefa Super Cup mara moja.
Pia aliifikisha Uholanzi katika nafasi ya pili ya Kombe la Dunia mwaka 2010, Hispania wakiwa mabingwa.
Kwa
upande wa Ribbery, amebeba ubingwa wa Bundesliga kwa misimu nane,
ameshinda Kombe la Ujerumani mara tano, akachukua Super Cup ya Ujerumani
mara moja, Ligi ya Mabingwa mara moja na Uefa Super Cup mara moja kama
ilivyo kwa Kombe la Dunia la klabu.
Riberry
naye aliiwezesha Ufaransa kushika nafasi ya pili Kombe la Dunia baada
ya kufungwa fainali na Italia, mechi ambayo Zinedine Zidane alilambwa
kadi nyekundu kwa kumtwanga kichwa Marco Materazzi.