Wabunge Waeleza Jinsi Walivyo na Hofu Kwa Sasa Kuihoji Serikali
Baadhi
ya wabunge wameeleza kuingiwa woga wa kuhoji na kudadisi masuala
mbalimbali kutokana na kutishiwa kutopatiwa fedha za miradi ya maendeleo
majimboni kwao.
Kauli
hiyo waliitoa wakati wakichangia semina ya wabunge juu ya jukumu la
Bunge katika kufuatilia kikamilifu matumizi ya Serikali yaliyofanyika
kwa kamati saba za Bunge.
Kamati
hizo ni Kamati ya Bajeti, Kilimo, Mifugo na Maji, Viwanda, Biashara na
Mazingira, Huduma za Jamii, Utawala na Serikali za Mitaa na Hesabu za
Serikali za Mitaa.
Akizungumza
katika semina hiyo, Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema
wabunge wamekuwa waoga kusemea tofauti na Bunge la 10 na kwamba hoja
zinajengwa kisiasa na wengine wanapohoji wanaambiwa hawatapelekewa fedha
majimboni.
Alisema
jambo linalowafanya wabunge kutosema yale wanayoyataka wananchi ni
siasa kuingia bungeni tofauti na mabunge yaliyotangulia ambapo wabunge
walikuwa wakiacha siasa lango kuu la kuingilia bungeni.
“Jambo
hili linaweza kuwa linasababishwa na viongozi wa bunge ama serikali
ambapo hoja zenye manufaa zinaweza kupelekwa bungeni, lakini wakaamua
kuziua,”alisema Selasini.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Mpendae (CCM) Salim Hassan Turky, alisema mambo
yote waliyoelezwa wanayajua, lakini kuna kitu kinachomoza bungeni na
kinaondoa uhai wa bunge.
“Hasa
unapohoji na kudadisi basi na wewe unaitwa na kuhojiwa na kudadisiwa,"
alisema Turky, "kwa hiyo wabunge wote wanakuwa waoga wa kuuliza
maswali".
"Sasa sijui kama utaratibu huu utafanya haki itendeke?”
Aliomba viongozi wa Bunge wakaliangalie hilo na kwamba endapo wakisimamia serikali vizuri wataweza kutekeleza majukumu yao.
Naye Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara alisema kuwa tatizo lililopo ni Bunge kutofanya kazi inavyotakiwa.
“Inafikia
Bunge mtu akisema hapana, waliosema hapana wasipewe fedha za maendeleo
kwenye majimbo yao wakati hayo mambo hayakuwapo,” alisema Mbunge huyo.
Alisema wabunge sasa wanaogopa kuisema au kuikosoa serikali licha ya kuwa Bunge limeundwa ili kusema kero za wananchi.
“Bunge
limebaki kuwa la muhuri na sio Bunge, na sisi hapa tunakuja kwa ajili
ya posho na mishahara tu tuliyoambiwa,” alisema Mbunge huyo.
Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM) alisema nguvu ya Bunge ya kuisimamia serikali ni ndogo kutokana na ukosefu wa fedha.
“Ili
tuweze kuwa na mchango madhubuti lazima tujengewe uwezo wa
kushughulikia taarifa mbalimbali, Bunge lihakikishe linatujengea uwezo
kwenye nyanja mbalimbali wabunge ili kuisimamia serikali ipasavyo kwenye
masuala mbalimbali ikiwamo bajeti,” alisema.
Mbunge
wa Ileje (CCM), Janet Mbene ambaye alikuwa mwenyekiti wa semina hiyo,
alisema kwa umoja wao wabunge wakisimama kwa pamoja serikali
itawasikiliza na hawatafanya kazi kwa woga.
