Hatima ya Zitto Kabwe na Kubenea Kutimuliwa Bungeni Au Kutotimuliwa Kujulikana Kuanzia Kesho
Mkutano
wa tisa wa Bunge la 11 utaanza vikao vyake kesho mjini Dodoma huku
kukiwa na hofu ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya chombo hicho cha
kutunga sheria kwa wabunge wawili Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) na Saed
Kubenea (Chadema).
Katika
mkutano uliopita wa chombo hicho cha kutunga sheria, Spika Job Ndugai
aliagiza wawili wakamatwe na polisi na kufikishwa mbele ya Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge akiwatuhumu kwa utovu wa nidhamu.
Zitto,
Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, alifika
mbele ya kamati hiyo na kujitetea, lakini kamati hiyo haikufanikiwa
kumhoji Kubenea baada ya Mbunge wa Ubungo huyo kufika mbele yake akiwa
anasukumwa kwenye kiti cha wagonjwa.
Kubenea
anadaiwa kulitumia Kanisa la Ufufuo na Uzima kumtuhumu Spika kusema
uongo bungeni kuhusu idadi ya risasi alizopigwa Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).
Kwa
upande wa Zitto, anadaiwa kumtuhumu Spika kukosea utaratibu alioutumia
katika kushughulikia ripoti mbili za uchunguzi wa almasi na tanzanite
akidai ripoti zake zilipaswa kujadiliwa bungeni.
Kutokana
na tuhuma hizo, kamati hiyo ya bunge inatarajiwa kutoa taarifa yake
kuhusu kuhojiwa kwa wabunge hao na hatima yao katika mkutano wa chombo
hicho utakaoanza kesho.
Masuala
mengine yanayotarajiwa kuwamo katika shughuli za vikao vya mkutano huo
ni pamoja na wabunge kujadili na kuishauri serikali kuhusu mapendekezo
ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali
katika mwaka wa fedha unaofuata.
Kwa
mujibu wa kifungu cha 94(1) cha Kanuni za Bunge, chombo hicho katika
mkutano wake wa Oktoba - Novemba kwa kila mwaka, kwa siku zisizopungua
tano, kinapaswa kukaa kama kamati ya mipango ili kukidhi matakwa ya
Ibara ya 63(3)(C) cha Katiba kwa kujadili na kuishauri serikali kuhusu
mapendekezo hayo.
Katika
mkutano huo, Bunge pia linatarajiwa kupokea, kujadili na kutoa maoni na
ushauri kuhusu mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya serikali.
Kifungu
cha 94(2)(b) cha Kanuni za Bunge kinabainisha kuwa Bunge katika mkutano
huo litapokea, kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu vyanzo vya
mapato vya serikali na pia litapokea, kujadili na kutoa maoni na ushauri
kuhusu mapendekezo ya utekelezaji wa mpango wa serikali na vipaumbele
kuhusu mpango huo.
Wabunge watapokea taarifa za utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa nusu mwaka kuanzia Julai hadi Novemba.
Katika
mkutano huo, Bunge linatarajia kujadili na kupitisha miswada mbalimbali
ukiwamo Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 4
wa mwaka 2017, Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano (TTCL) wa
mwaka 2017 na Muswada wa Uwakala wa Meli Tanzania.
Bunge
pia linatarajiwa kuutumia mkutano huo kutapokea taarifa za utekelezaji
wa kamati zake katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/18.
