HATARI YA KULA UDONGO UNAOPENDWA NA WAJAWAZITO ' UDONGO WA PEMBA'
Wanawake
wanaopenda kutafuna udongo maarufu kwa jina la pemba na hasa wakati wa
ujauzito wanapaswa kufikiria mara mbili kabla ya kufanya hivyo.
Hii ni kutokana na watafiti nchini kubaini kuwa viwango vya madini ya
kemikali katika udongo huo nchini vimezidi kipimo kilichowekwa na
Shirika la Afya Duniani (WHO).
Utafiti uliofanywa katika mikoa 12 ya Tanzania na wanasayansi kutoka
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Bugando (Cuhas-Bugando)
wakishirikiana na wenzao kutoka Canada na Marekani, umebaini madini kama
vile lead (risasi), arsenic, cadmium, nickel na aluminiamu katika
udongo huo yanahatarisha afya za akinamama hao na watoto ambao
hawajazaliwa.
Utafiti huo ambao umekamilika mwaka huu umefanywa kwa kipindi cha miaka
mitano katika mikoa ya Singida, Rukwa, Lindi, Dodoma, Mbeya, Kusini
Pemba, Mara, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Tanga na Ruvuma.
Hata hivyo, mtafiti mkuu katika utafiti huo, Elias Nyanza kutoka Cuhas
amesisitiza kuwa wao wamejikita katika kuchanganua udongo unaouzwa
katika masoko.
“Hatuna shida na uuzwaji wa udongo huu. Kinachotutia hofu ni viwango vya
madini ya kemikali tulivyobaini na vyanzo vya udongo huo,’’ alisema
Nyanza katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi.
“Tulichukua sampuli za udongo kutoka maeneo mbalimbali ya uzalishaji
katika mikoa 12 ya Tanzania. Tuliuchanganua udongo huo kwa kutumia
utaalamu wa kimaabara uitwao ICP-MS.’’
Alisema utafiti huo uko katika mchakato wa kuchapishwa katika majarida ya kisayansi kimataifa.
“Tunashauri ulaji wa udongo huu uzuiwe hadi pale walaji
watakapohakikishiwa usalama wao kiafya,’’ alisema Nyanza ambaye ni
mtaalamu wa afya ya mazingira kutoka Shule Kuu ya Afya ya Jamii,
Cuhas-Bugando. Nyanza alishirikiana na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha
Colorado Denver cha Marekani na cha Calgary, Canada. Alisema madini
waliyoyabaini kama vile risasi, cadmium na arsenic tayari yameorodheshwa
na shirika la Marekani la viambata vyenye sumu na magonjwa.
Mtafiti huyo alisema madini hayo yanajulikana kwa kusababisha madhara
kiafya na hasa kwa mama na mtoto, hata yakiwa katika kiwango kidogo.
“Madini mengi ya kemikali, hasa yale tuliyochanganua kutoka kwenye
udongo unaoitwa pemba yako katika viwango vya juu kuliko inavyotakiwa
katika miongozo ya Shirika la Afya Duniani,’’ alisema.
Nyanza alisema, “Kuna wanawake tulikuta wanakula udongo wenye viwango
vya madini hayo kufikia 50 micrograms per litre hadi 60 micrograms per
litre, lakini WHO inasisitiza kuwa madini haya yanakuwa salama pale
yanapotumika katika viwango vya 10 micrograms per litre.’’
“Ulaji wa udongo huu unaongeza hatari ya wanawake kuzaa watoto wafu,
wenye uzito mdogo, njiti na hata wakati mwingine kusababisha watoto
kuzaliwa wakiwa na hitilafu za kimaumbile,’’ alitahadharisha Nyanza.
Mkemia mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyere amependekeza watafiti
hao wachukue sampuli walizozipata katika utafiti na kuziwasilisha katika
ofisi yake ili hatua za kuingilia kati suala la udongo huo zitekelezwe
ipasavyo na mamlaka zinazohusika.
“Sisi katika maabara ya mkemia mkuu bado hatujafanya utafiti kama huo.
Ila tuna teknolojia ya kuweza kubaini hicho wanachodai wamekuta katika
udongo huo. Wataarifu walete sampuli walizokusanya ili nasi tujiridhishe
kwanza,’’ alisema Profesa Manyere alipozungumza na mwandishi wa gazeti
hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam kuhusu utafiti huo.
“Mojawapo ya madini yanayotajwa hapo ni risasi ambayo kweli ni hatari
kwa afya. Sisi tuko katika mchakato wa kuyawekea miongozo lakini si
katika ulaji wa udongo.”
Maeneo ya uchimbaji dhahabu
“Hatari zaidi tuliibaini kwa wanawake wanaokula udongo unaotengenezwa
kutoka ardhi iliyopo maeneo ambayo kuna shughuli za wachimbaji wadogo wa
dhahabu,’’ alisema Nyanza.
Mwaka 2014, utafiti mwingine uliofanywa katika maeneo yenye shughuli za
uchimbaji madini ulionyesha kati ya wanawake 115 walioshirikishwa,
asilimia 69 walinunua udongo (pemba) huo kutoka kwenye maduka na
asilimia 31 walikula udongo maarufu kama kichuguu. “Kwa pemba na
kichuguu, utafiti huo uligundua viwango vikubwa vya arsenic, chromium,
shaba, chuma, manganizi, nickel na zinki. Viwango vya cadmium na zebaki
vilikutwa zaidi katika sampuli za kichuguu,’’ watafiti walisema katika
Jarida la BMC Pregnancy and Childbirth utafiti ulikochapishwa.
Katika utafiti huo, watafiti walishauri hatua za kiafya zichukuliwe
kunusuru afya za akinamama wanaokula udongo unaozalishwa kutoka maeneo
ya migodi.
“Hatua za kisera na programu za kuelimisha zichuliwe katika mazingira ya
wachimbaji wadogo, wanawake wanazidi kula udongo na wanajiweka katika
hatari kiafya,’’ wanaeleza watafiti katika mapendekezo yao.
Pia, walisema sababu zinazowafanya wanawake kula udongo zichunguzwe na elimu itolewe katika kukabiliana na hatari za kiafya.
Wengi wanaamini ulaji wa udongo huwasaidia kutatua changamoto za
ujauzito kama vile kichefuchefu, upungufu wa madini ya chuma na wakati
mwingine wanakuwa na hamu tu ya kuula.
Dk Latifa Kalinga kutoka Hospitali ya Mkoa ya Songwe, alisema kwa uzoefu
wake wa kidaktari na mwanamke aliyewahi kuwa mjamzito, kula udongo ni
kati ya changamoto zinazowakumba wengi. “Ujauzito huwa na changamoto
nyingi. Wakati mwingine wanawake hupenda tu kula udongo. Wanaweza kula
hata barafu katika jokofu, kutafuna mchele kilo nzima na mengine. Hii
tabia inaitwa pica katika lugha ya kitaalamu,’’ alisema huku akisisitiza
inapaswa washauriwe waache kwa kujiweka katika hatari ya kupata minyoo
inayosababisha upungufu wa damu
Imeandikwa na Syriacus Buguzi - Mwananchi Mwanza