UVCCM Yawapa ONYO BAVICHA......Yadai Tundu Lissu si Mtu wa Kwanza Kupigwa Risasi
Uongozi
wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umesema mwanasheria
wa Chadema, Tundu Lissu si kiongozi wa kwanza kupigwa risasi, hivyo
vyombo vya dola viachwe vifanye upelelezi.
Lissu
alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi tano Alhamisi wiki hii nyumbani
kwake Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu jijini Nairobi,
Kenya.
Kaimu
Katibu Mkuu wa umoja huo, Shaka Hamdu Shaka amesema hayo jana Jumapili,
akilitaka Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) lisione kwamba wao ndio
wameguswa na tukio la Lissu kupigwa risasi kuliko Watanzania wengine.
“Ukweli ni kwamba sote tumeguswa na tukio hilo, jambo la msingi ni kuviachia vyombo vya Dola vifanye upelelezi,” amesema.
Shaka amesema kuna viongozi wengine walikufa kwa kupigwa risasi na uchunguzi ukafanyika kupitia vyombo vya ulinzi na usalama.
Kauli
ya UVCCM imetolewa baada ya Bavicha kukaririwa ikiitaka Serikali kuunda
tume huru itakayochunguza matukio ya uvunjifu wa amani likiwemo la
kupigwa risasi Lissu.
Bavicha
imesema tume hiyo inapaswa kuihusisha Chadema kwa kuwa viongozi wake
wengi wamekumbwa na vitendo hivyo. Shaka amesema Bavicha iache kuingilia
utaratibu wa upelelezi.
Amesema Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume aliuawa kwa kupigwa risasi.
Kiongozi mwingine aliyeuawa kwa risasi amesema ni naibu waziri katika Serikali ya Awamu ya Pili, Nicas Mahinda.
Katika
duru za kimataifa, Shaka alitoa mfano wa aliyekuwa Rais wa Marekani,
John F. Kennedy na Rais wa Misri, Anuar Saadat ambao waliuawa kwa
kupigwa risasi.
“Matukio
ya ujambazi yanayofanywa na watu wasiojulikana hutokea hata katika
mataifa makubwa na mara nyingi upelelezi wake huchukua muda mrefu kwa
wahusika kukamatwa,” amesema.
Amesema Bavicha waache kuyahusisha matukio makubwa yanayochukua uhai wa watu na masuala ya kisiasa.
Shaka
amesema UVCCM inamuunga mkono Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
aliposema huu si wakati wa kunyoosheana vidole vya lawama bali viachiwe
vyombo vya usalama vitimize wajibu wake.
“Mbowe ametamka matamshi yaliyopevuka kifikra, kiupeo na kisiasa,” amesema Shaka.
Alisema Bavicha wasitumie tukio la Lissu kupigwa risasi kama jukwaa lao la kufanya siasa.
"Umoja
wa vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM tunawakanya BAVICHA na kuwataka
waache tabia ya viherehere ya kuingilia taratibu za kitawala na
upelelezi pindi yanapotokea masuala mazito yanayohusisha maisha ya watu,
kushambuliwa au kutekwa na wao wakataka kuyageuza kuwa ya kisiasa.
BAVICHA wamejaribu kuyaunganisha matukio kadhaa walioyaita yamefanywa na
watu wasiojulikana bila ya kufanya upelelezi wa aina yeyote na kutaja
baadhi ya majina ya watu waliyokumbwa kwenye matukio hayo na kukwepa
kutaja mfululizo wa mauaji ya viongozi wa CCM na serikali huko Kibiti
mkoani Pwani", alisema Shaka.
Shaka
alisema umoja huo unashauri wananchi wakaongozwa kwa busara kuliko
ushabiki ambao unaweza kuliingiza Taifa katika machafuko.
