Mbowe Aeleza Alipo Dereva wa Tundu Lissu
Mwenyekiti
wa (CHADEMA) Freeman Mbowe amefunguka na kuweka wazi sehemu alipo
dereva wa Tundu Lissu ndugu Simon Mohamed Bakari na kusema kwa sasa yupo
nchini Kenya akipatiwa huduma za kisaikolojia kufuatia kushuhudia tukio
hilo la kinyama.
Mbowe
amesema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari ambapo ameweza
kuzungumzia mambo mbalimbali kuhusu sakata hilo na kusema kuwa waliona
ni busara kumchukua dereva huyo na kuwa naye nchini Kenya kwa ajili ya
kupatiwa msaada huo hadi watakapooona hali yake ya kiafya na uhakika na
usalama wake ndiyo anaweza kurejea nchini Tanzania.
"Dereva
wa Mhe. Lissu, Simon Mohamed Bakari naye tunaye hapa Nairobi akiendelea
kupata huduma za kisaikolojia. Alishuhudia shambulio lile na aliokoka
kimiujiza. Anasumbuliwa na msongo mkubwa wa mawazo. Naye hatukuona
busara kuendelea kumwacha nchini hadi hapo hali yake ya kiafya na
kiusalama itakapohakikishwa. Ni dhahiri kwa aina ya shambulio
lilivyokuwa, wauaji walikusudia kuwauwa wote, Mhe. Lissu na hata Dereva
wake" alisema Freeman Mbowe
Mbali
na hilo Mbowe amewataka wabunge wa upinzani kuwa na tahadhari kubwa
akidai kuwa kama wasipokuwa makini huenda kiongozi mwingine anaweza
kupata matatizo kama hayo hata hivyo amesema kuwa tamko la chama chake
litakuja karibuni.
"Tutamuenzi
Baba wa Taifa aliyetuasa: “tukiwa waoga tutatawaliwa ma madikteta!”
Wabunge na Viongozi wa Upinzani ndiyo “Target”. Nawasihi viongozi na
wabunge wetu wachukue kila tahadhari. Wanachama nao wawe tayari kulinda
na kupigania wajibu wetu, usalama wa viongozi na chama chetu kwa
ujasiri. Tusipochukua hatua, kesho atadhurika mwingine!Tamko na agizo
rasmi la Chama litafuata karibuni" alisema Freeman Mbowe.
Freman
Mbowe amedai kuwa Tanzania si sehemu salama tangu umefanyika Uchaguzi
Mkuu mwaka 2015 na kudai kuanzia hapo yalianza kujitokeza kwa mauaji ya
viongozi kikiwepo kifo cha Mhe. Alphonce Mawazo Mkoani Geita, Kupotea
kwa kina Ben Saanane. Kutekwa wasanii na kufanyiwa mateso makubwa
pamoja na Wabunge kufungwa na kushtakiwa kila siku.
