Serikali yawaonya waajiri kuhusu wafanyakazi wanaonyonyesha
Serikali imeonya waajiri wanaoweka vikwazo kwa wafanyakazi wao wanaonyonyesha watoto walio chini ya miezi sita.
Onyo
hilo limetolewa leo Jumanne na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati anafungua maadhimisho ya
wiki ya unyonyeshaji duniani.
"Serikali
ya awamu ya tano katika kuhakikisha watoto wanakuwa na afya bora,
imeweka kanuni inayompa nafasi ya saa mbili mama mwenye mtoto wa chini
ya miezi sita kumnyonyesha mwanaye," amesema Waziri Mwalimu.
Amesema
kutokana na kanuni hiyo, waajiri wanapaswa kuwapa ushirikiano mzuri
akina mama hao, kwa kuwa maziwa ya mama ndiyo msingi wa afya bora ya
mtoto.
Waziri
Mwalimu amebainisha kuwa ili mtoto aweze kuwa na afya bora, anapaswa
kunyonya maziwa ya mama kwa miezi sita mfululizo bila kinywaji au
chakula kingine chochote.
Mkurugenzi
Mtendaji wa taasisi ya Chakula na Lishe, Dk Joycline Kaganda, amesema
maadhimisho haya hufanywa kila mwaka kuanzia Agosti 1 hadi 7.
"Maadhimisho haya yanalenga kusisitiza umuhimu wa kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa ya mama," amesema
Katika
maadhimisho hayo, programu ya huduma ya taarifa za lishe kupitia simu
za mkononi (M-Nutrition) imezinduliwa. Progrtamu hiyo inakusudia kuleta
mabadiliko ya tabia kuhusu afya na lishe ya watoto, wanawake wajawazito
na wanyonyeshao.