Naibu Waziri Atoa Maagizo Mazito kwa Polisi Kitengo cha Madawa ya Kulevya
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mh Hamad Masauni amewaagiza askari wa
Kitengo cha kudhibiti dawa za Kulevya kote nchini kuwasilisha ripoti ya
ukamataji wa dawa za kulevya katika maeneo yao baada ya kubaini kuwepo
kwa utendaji kazi usioridhisha
Akizungumza
mara baada ya kutembelea kitengo cha Polisi cha Kudhibiti Dawa za
Kulevya kilichopo Kilwa Road Jijini Dar es Salaam, Mh. Masauni amesema
kuwa, taarifa iliyopo ya ukamataji na udhibiti wa dawa hizo hauridhishi,
na kutaka ripoti za maeneo mbalimbali nchini ziwasilishwe ili kupima
utendaji kazi wa kitengo hicho katika kudhibiti dawa hizo zilizopigwa
marufuku hapa nchini.
Mh.
Masauni, amesema kuwa hawawezi kufumbia macho suala hilo kwani kuna
baadhi ya maeneo yanasifika kwa kuwepo kwa dawa hizo akitolea mfano Mkoa
wa Mjini Magharibi Zanzibar wenye matumizi makubwa ya dawa za kulevya
lakini takwimu za udhibiti zipo chini.
Mh.
Masauni amesema kuwa, Serikali inafanya jitihada za kila siku kudhibiti
suala la uingizwaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya hususani
maeneo ya mipakani na bandari zote kwani wanalenga kudhibiti kwa
kiwango cha juu upatikanaji wa dawa hizo hapa nchini.