Makamba: Serikali haina nia ya kurudisha viroba
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January
Makamba amesema Serikali haina nia ya kurudisha sokoni pombe
zilizotengenezwa katika mifuko ya plastiki 'viroba' na kuwataka
Watanzania kupuuza uzushi unaoenezwa kwamba pombe hizo zitarudi.
Makamba
alitoa kauli hiyo jana, Jumatatu Agosti 14 alipotembelea eneo la Kimara
Temboni lilipo ghala la kuhifadhi pombe mbalimbali ikiwamo viroba
linalomilikiwa na Kampuni Thema.
Makamba
alisisitiza kwamba Serikali uamuzi wake wa kuzuia pombe hizo upo
palepale na haujabadilika hivyo watu waache kupotosha wenzao.
"Baada
ya kupiga marufuku kuna kampuni zilikuja ofisini kuomba kuongezewa
muda, lakini tuliwakatalia na kuwaambia waheshimu uamuzi uliotolewa sasa
hizi tetesi ya kwamba vinarudi sokoni sijui zinatoka wapi," alisema Makamba.
Makamba
ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli amesema njia ya pekee kwa
wafanyabiashara hao wa viroba wanaotakiwa kuifanya ili kupunguza hasara
ni kubadilisha pombe hizo na kuziweka katika chupa zenye ujazo
unaotakiwa.
Amesema kamwe Serikali haiwezi kurudi nyuma na kwamba mafanikio yameanza kuonekana kutokana na hatua hiyo.
