Mahakama Yazuia Bomoabomoa kwa nyumba 286 Dar
Wakati
operesheni ya ubomoaji wa nyumba zilizoko ndani ya umbali wa mita 121.5
kutoka katikati ya Barabara ya Morogoro ikiendelea maeneo ya Kimara
mpaka Kiluvya jijini Dar es Salaam, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi
imeziwekea kinga ya muda nyumba 286 zinazohusika.
Uamuzi
huo wa Mahakama ulitolewa juzi na Jaji Leila Mgonya kutokana na maombi
ya zuio yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakazi hao 286 wa maeneo ya
Ubungo- Maji hadi Kiluvya wakiomba itoe zuio la muda hadi kesi yao ya
msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Maombi
hayo ya zuio la muda kusubiri uamuzi wa kesi ya msingi yamepangwa
kusikilizwa Agosti 30 baada ya upande wa wajibu maombi (Serikali)
kuwasilisha hati ya kiapo kinzani.
Hata
hivyo, wakati wakisubiri usikilizwaji wa maombi ya zuio la muda,
wananchi hao kupitia kwa wakili wao, Benito Mandele waliwasilisha maombi
ya dharura wakioomba mahakama hiyo iamuru hali iendelee kuwa kama
ilivyo kwa sasa hadi maombi hayo yatakaposikilizwa.
Jaji
Mgonya anayesikiliza shauri hilo alikubaliana na maombi hayo na kuamuru
hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi tarehe hiyo ya maombi hayo
yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Kwa
uamuzi huo, Tanroads ambayo ndiyo mtekelezaji wa operesheni hiyo
haitaweza kuzigusa nyumba hizo hadi hapo mahakama itakavyoelekeza
vinginevyo baada ya usikilizwaji wa maombi hayo ya zuio la muda kusubiri
kesi ya msingi kumalizika.
Wakili
Mandele alisema kuwa watakachofanya baada ya kupata hati ya amri hiyo
ya mahakama wataitoa nakala nyingine na kuwagawia kila mdaiwa kwa ajili
ya kuiweka kwenye nyumba yake.
Katika
kesi ya msingi namba 284 ya mwaka 2017, wananchi hao wanaiomba mahakama
itamke kuwa wao ni wamiliki halali wa maeneo hayo yenye mgogoro na
kwamba hawapo katika hifadhi ya barabara.
Pia,
wanaiomba mahakama hiyo iamuru kuwa kama Serikali inata kuwahamisha na
kuyachukua maeneo yao, basi iwalipe fidia stahiki kwa mujibu wa sheria.
Tanroads
imetoa notisi kwa wakazi wote walipo katika umbali wa mita 121.5 kutoka
katikati ya barabara ya Morogoro kila upande, kuanzia Ubungo - Maji
hadi mpakani mwa Dar es Salaam na Pwani kuvunja nyumba zao kwa madai
kuwa wapo kwenye hifadhi ya barabara.
Hivyo, Tanroads waliwataka wananchi hao kuondoka katika maeneo hayo ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
Wananchi
hao wanapinga amri hiyo wakidai kuwa wanaishi katika maeneo hayo
kihalali kwa kuwa wana hatimiliki halali na hawapo kwenye hifadhi ya
barabara, huku wakihoji sheria iliyotumika kuidhinisha umbali huo wa
mita 121.5.
Kutokana
na hali hiyo, wananchi hao wameamua kwenda mahakamani katika makundi
tofauti na kufungua kesi tofautitofauti kupinga operesheni hiyo wakidai
kulipwa fidia kama Serikali itawahamisha.
Mbali na kesi hiyo iliyotolewa amri hiyo, pia kuna kesi nyingine mbalimbali ambazo ziko katika hatua mbalimbali.
Kesi
hizo nyingine ni ile iliyofunguliwa na Abdallah Maliki kwa niaba ya
wenzake 570 ambao ni wakazi wa maeneo ya Kimara, Mbezi na Kiluvya dhidi
ya Tanroads na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa upande mwingine.
Shauri
jingine ni maombi ya kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi kupinga
operesheni hiyo lililofunguliwa na Ephrahim Kavishe na wenzake wanne ili
wawe wawakilishi wa wenzao zaidi ya 198 ambao ni wakazi wa Kimara Stop
Over na Mbezi.
Hata
hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mmoja wa wajibu maombi
hayo amewawekea pingamizi akiiomba mahakama hiyo iyatupile mbali maombi
hayo huku akiainisha kasoro mbalimbali za kisheria.
Maombi
hayo yanasikilizwa na Jaji Crencecia Makuru na amepanga kutoa uamuzi
kuhusu pingamizi hilo Agosti 30, uamuzi ambao ndio utakaotoa hatima ya
maombi hayo kama yataendelea kusikilizwa au yatatupiliwa mbali.