Mahakama Yaigomea TRA Kumhoji Manji
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu leo August 9, 2017 imeukatilia upande wa
Serikali kutaka Mfanyabiashara Yusuf Manji ahojiwe na Mamlaka ya Mapato
Tanzania, TRA kuhusu masuala ya kodi.
Maombi
ya kutaka Manji ahojiwe na TRA, yamewasilishwa mbele ya Hakimu
Mfawidhi, Cyprian Mkeha na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi
Mutalemwa ambaye amedai wanaiomba Mahakamani itoe kibali ili Manji
ahojiwe kisha atarudisha ndani ya muda wa kazi kabla haujaisha.
Hata
hivyo, Wakili anayemtetea Manji, Alex Mgongolwa amedai ombi hilo sio
sahihi kwa kuwa walikwishafanya mawasiliano ya maandishi na TRA na
kusema kuwa wapo Mawakili wa Manji wanaoshughulika na masuala ya kodi na
siyo wao hivyo anahitaji kuwasiliana nao ili mahojiano hayo yawe na
manufaa.
Kutokana
na hatua hiyo, Kishenyi amedai anayehitajiwa ni Manji siyo Makampuni
yake na kwamba akifika huko na kuona ipo haja ya kuwa na wataalam wake
atasema.
Hakimu
Mkeha amesema hawezi kuruhusu ombi hilo kwa sababu kesi iliyopo mbele
yake ni ya uhujumu uchumi ambayo haihusiani na masuala ya kodi hivyo
ameahirisha kesi hadi August 18, 2017 kwa ajili ya kutajwa.