Jukwaa la Wahariri (TEF) Waondoa Zuio La Kutotangaza Habari Za Mkuu Wa Mkoa Wa Dar Es Salaam, Paul Makonda.
Jukwaa
la Wahariri (TEF) leo limetangaza kuondoa zuio la kutangaza habari za
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda huku yeye akikataa kuomba
radhi na kusema kuwa yaliyopita yamepita na sasa tugange yajayo.
Hayo
yameibuka leo katika mkutano wa pamoja wa Makonda na TEF, ambao hapo
awali walitangaza uamuzi wa kutoshirikiana na Mkuu huyo wa Mkoa kwa
kutotangaza habari zinazomhusu kufuatia madai ya kuvamia kituo cha
luninga cha Clouds Media Group na kumtaka aombe radhi.
Kwa
mujibu wa Katibu wa TEF, Theophil Makungu, Makonda amekiri kuwa tukio
hilo lilitokea lakini dhana ya wakati tukio lilipotokea haikuwa kama
ilivyochukuliwa lakini akamtaka kuomba radhi.
Hatahivyo Mkuu huyo wa Mkoa alikataa kuomba radhi kama ambavyo TEF ilikuwa inataka tangu awali.
“Ndugu waandishi wa Habari na Wahariri, kile ambacho Katibu amekisema hakitatokea kwenye kinywa changu, sitaomba radhi,” amesema Makonda.
TEF
imesema kuwa walichokisikia mara ya kwanza kilitoka Clouds lakini
hawakupata nafasi ya kusikiliza kutoka kwa Mkuu wao wa Mkoa na hivyo
mahusiano kati ya waandishi wa habari na yeye (Mkuu wa Mkoa) yaende
vizuri kuanzia sasa na kuendelea.
Wakati
huohuo, Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge
Mutahaba amesema kuwa TEF haiwezi kusema kuwa ilipokuwa inazungumza na
Mkuu wa Mkoa, haikupata upande wa pili, upande wa pili ulikuwepo na
jambo hili liliripotiwa.
“Hatuko sawa kwasababu kwanza TEF haijawahi kutafuta nafasi ya kusikiliza upande wangu,” amesema Ruge.
Haya
yanajiri siku chache baada ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuwaita
jukwaani Makonda na Ruge na kuwataka kumaliza tofauti zao kwa kushikana
mikono.