KOCHA AZAM FC ANAAMINI WAKIREJEA KUTOKA UGANDA, KAZI MNAYO
KIKOSI CHA AZAM FC MSIMU ULIOPITA
Kocha
Mkuu wa kikosi cha Azam, Aristica Cioaba raia wa Romania ameweka wazi
kuwa makali ya kikosi chake hicho yataongezeka baada ya kurejea nchini
wakitokea Uganda ambapo wameenda kuweka kambi.
Azam
wamekimbilia nchini Uganda kuweka kambi ya wiki mbili ya kujiandaa na
msimu mpya wa ligi utakaoanza Agosti 26, mwaka huu ambapo wakiwa huko
watacheza mechi za kirafiki na timu za KCCA, Vipers, URA na Onduparaka.
Mromania
huyo amesema kuwa kambi hiyo ya nje ya Tanzania waliyoipata
itakiwezesha kikosi chake kujinoa kwa utulivu na kuwasaidia nyota wake
kuungana kwa pamoja na kutambuana wanavyocheza, jambo ambalo litasaidia
kutimiza kile ambacho anakitaka kwenye msimu ujao.
“Kambi
ya huku Uganda ina faida kubwa kwetu, na labda nikuhakikishie kuwa
tukitoka huko tutakuwa moto wa kuotea mbali kwenye ligi kuu kwani
wachezaji wangu watakuwa wameshika kile nitakachowafundisha kwa kiasi
kikubwa.
“Unajua
mnapokuwa nje mnapata nafasi ya kuwa huru kufundisha mbinu zako
kiutulivu kwa sababu hauna hofu labda watu fulani watakuona kile
unachokifundisha, lakini hii ndiyo mara ya kwanza kwa wachezaji wote
kuwa sehemu moja, jambo ambalo litafanya wachezaji kujuana kwa urahisi
tofauti na muda mwingine tulipokuwa tunajinoa,” alisema Mromania huyo.