KAMA ULITAKA KUIINGIZA YANGA MJINI NA WACHEZAJI "MAGARASA", SAFARI HII SAHAU...
Mabingwa
wa Tanzania, Yanaga sasa wameweka wazi kuwa, wapo makini kuelekea
dakika za mwisho za usajili wa wachezaji wa kigeni kwa kuhakikisha
hawasajili magarasa kama ilivyotokea huko nyuma kwa mitego waliyokuwa
wakiwekewa.
Usajili
kwa wachezaji raia wa Tanzania umemalizika tangu Agosti 6, mwaka huu,
lakini Yanga ina nafasi ya kusajili mchezaji mmoja wa kigeni hadi Agosti
15 ambapo usajili huo utafungwa.
Katibu
Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa amesema kipindi hiki wameamua kuwa
makini zaidi ili kuepuka kusajili wachezaji wenye uwezo mdogo ambao
huwaghalimu.
“Kuna
wachezaji walikuja kwa ajili ya kufanya majaribio na tumeona hawana
uwezo hao ni Mnigeria, Henry Okoh na Mcameroon, Ferdinand Bongyang
ambaye tunamrudisha kwao muda wowote.
“Kwa
sasa amebaki Yisa Mfowoshe ambaye ni Mnigeria huyu anaendelea
kuangaliwa na tunasubiri majibu ya benchi la ufundi kama wameridhika
naye ndiyo tujue mchakato wa kumsajili.
“Kumekuwa
na tabia za mawakala kuleta wachezaji katika dakika za mwisho kwa ajili
ya kufanya majaribio ambapo wamekuwa wakiangaliwa haraka haraka kisha
wanasajiliwa.
“Huu
ni mtego unaofanywa makusudi ili tuwasajili haraka bila kutathimini kwa
kina uwezo wao, sasa tumeamua kuwa makini zaidi na suala hilo ili
kusajili wachezaji wenye viwango na si vinginevyo,” alisema Mkwasa.
Wakati
huohuo, kiungo mkabaji wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi anatarajiwa
kuwasili nchini leo Jumamosi tayari kukitumikia kikosi hicho.
Tshishimbi raia wa DR Congo anawasili nchini baada ya Yanga kumalizana na klabu yake ya Mbabane Swallows ya Swaziland.