DPP AAMUA KUACHANA NA KESI YA UGAIDI DHIDI YA MBUNGE WA CHADEMA WILFRED LWAKATARE
Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ameondoa maombi yake dhidi
ya Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare kuhusiana na
shtaka la ugaidi dhidi yake.
DPP alikuwa amefungua maombi Mahakama ya Rufani akiomba kibali cha
kufungua maombi ya mapitio kuhusiana na uamuzi wa Mahakama Kuu kumfutia
Lwakatare mashtaka ya ugaidi.
Maombi hayo ya DPP yalitarajiwa kusikilizwa leo Ijumaa, Agosti 11 na
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mussa Kipenka, lakini DPP akaamua kuyaondoa
kabla ya usikilizwaji.
Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka ameieleza mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea na maombi hayo.
Kutokana na nia hiyo ya DPP, wakili wa mjibu maombi, Richard Rweyongeza
amesema kuwa hana pingamizi dhidi ya nia ya DPP kuyaondoa maombi hayo na
Jaji Kipenka akatoa amri ya kuyaondoa mahakamani maombi hayo.
Kwa uamuzi huo sasa Lwakatare anabaki na shtaka la kula njama ili
kutenda kosa, katika kesi ya msingi inayosikilizwa na Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu.
Awali, Lwakatare na mwenzake walikuwa Ludovick Rwezaura walikuwa
wakikabiliwa na jumla ya mashtaka manne likiwemo la kula njama za
kufanya vitendo vya kigaidi kwa lengo la kumdhuru kwa sumu aliyekuwa
Mhariri wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky.
Mashtaka mengine yalikuwa ni ya ugaidi, wakidaiwa kuandaa mikutano ya
kupanga makosa ya kigaidi na kufadhili vitendo vya kigaidi.
Hata hivyo, Lwakatare kupitia kwa mawakili wake walifungua maombi
Mahakama Kuu wakipinga mashtaka hayo yaliyokuwa yakiangukia katika
Sheria ya Ugaidi.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Lawrence Kaduri
ilikubaliana nayo na akamfutia Lwakatare mashtaka hayo ya ugaidi na
hivyo kubakiwa na shtaka moja tu la kula njama ambalo haliangukii katika
sheria hiyo ya ugaidi.
DPP hakukubaliana na uamuzi huo wa Mahakama Kuu, ndipo akafungua maombi
ya kibali kufungua maombi nje ya muda, ili kupinga uamuzi wa Mahakama
Kuu kumfutia mashtaka hayo ya ugaidi.
