Chadema Yamlima Barua Kaimu Jaji Mkuu
Kamati
Kuu ya Chadema imemwandikia barua Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma
kulalamikia kitendo cha mahakama nchini kuwanyima dhamana wanachama
wake wanapofikishwa mahakamani.
Akiwasilisha
azimio la Kamati Kuu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah
Safari amesema wanamtaka aingilie kati suala hilo na kuhakikisha kwamba
makosa yanayodhaminika basi yanapewa dhamana.
Profesa
Safari amesema katika barua hiyo wamebainisha kesi tano za viongozi na
wanachama wa Chadema ambao wamenyimwa au kucheleweshewa dhamana zao
kwenye mahakama mbalimbali.
"Hivi
ndiyo vitu ambavyo Jaji Mkuu anatakiwa kivifahamu, yeye ndiye custodian
wa uhuru wa Mahakama. Ninaamini kwamba atalifanyia kazi suala hili,"
amesema Profesa Safari.
Baadhi
ya kesi zilizobainishwa kwenye barua hiyo ni pamoja na kesi ya jinai
kati ya Jamhuri na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na
wenzake wanane huko Songea.
Kesi
nyingine ni jinai dhidi ya wajumbe wa Serikali ya Mtaa huko Mbozi
pamoja na wanachama wengine wawili; jinai dhidi ya Maduka Michael Maduka
na wenzake 51 huko Chato.
Pia,
ipo kesi ya jinai dhidi ya Tundu Lissu na Godbless Lema ambao wote
walinyimwa dhamana kwa madai kwamba hakukuwa na sababu za msingi kwa wao
kunyimwa dhamana.