Waziri Mkuu: Ufuta Kuuzwa Kwa Mfumo Wa Stakabadhi Ghalani
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imemuagiza Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba akutane na Bodi ya mazao
mchanganyiko kwa ajili ya kuliondoa zao la ufuta na kuliingiza katika
mfumo wa stakabadhi ghalani.
Pia
amewaagiza wakuu wa mikoa yote inayolima zao la ufuta kukutana na Dkt.
Tizeba kwa ajili ya kupanga mfumo mzuri wa uuzaji katika msimu wa mwaka
2016/2017 wakati Serikali ikijipanga kuliingiza zao hilo katika mfumo wa
stakabadhi ghalani.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Julai 10, 2017) wakati
akisalimiana na wananchi katika vijiji vya Nangano, Kibutuka na Kiangara
alipowasili katika wilaya ya Liwale kwa ajili ya ziara ya kikazi ya
siku nne mkoani Lindi.
Ametoa
kauli hiyo baada ya mbunge wa jimbo la Liwale, Mheshimiwa Kuchauka
pamoja na wananchi kuiomba Serikali iwasaidie kuboresha bei ya zao la
ufuta ambayo imekuwa ikiyumba.
Waziri
Mkuu amesema “tatizo lipo kwenye mfumo wa uuzaji zao la ufuta, unauzwa
kwa bei ya rejareja, wanunuzi wako huru. Serikali imemuagiza Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuliondoa zao katika bodi ya mazao mchanganyiko
na kuliingiza katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuboresha bei
yake.”
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Liwale Bw. Justine Monko kuhakikisha anamaliza tatizo la maji
katika vijiji vya Nangano,Kibutuka na Kiangara.
Amesema
Serikali imedhamiria kuondoa tatizo la maji kwa kuhakikisha kuwa
wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi
mita 400. “Ndio maana Serikali imekuja na Kampeni inayosema mtue mama
ndoo kichwani.”
Pia
amemtaka Mhandisi wa Maji Bw. Andrew Kilembe kuandika barua ya
kufuatilia fedha za maji sh. milioni 76 kwa ajili ya kijiji cha Kiangara
walizopangiwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa Waziri wa Maji ili
waweze kukamilisha uchimbaji wa kisima.