Waziri Mkuu: Hakuna Mgonjwa atakayetibiwa bila kupatiwa dawa
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili
ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kwamba hakuna mgonjwa atakayekwenda
kutibiwa katika hospitali, vituo vya afya au zahanati bila ya kupatiwa
dawa.
Ameyasema
hayo juzi jioni (Jumatatu, Julai 10, 2017), wakati akizungumza na
wananchi wa wilaya ya Liwale katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye Uwanja wa Michezo wa Wilaya.
Waziri
Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa katika ziara yake
ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi, alisema Serikali haitaki kusikia
wananchi wanakwenda hospitali, Vituo vya afya au zahanati na kukosa
dawa.
Alisema
moja kati ya ajenda muhimu ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuboresha
huduma za afya kwa wananchi wake, ambapo kila mwezi halmashauri zote
nchini zinapelekewa fedha za ununuzi wa dawa.
“Serikali
hii ya Rais Dkt. John Magufuli inatoa fedha za kununulia dawa kila
mwezi katika halmashauri zote nchini. Sasa kama hapa Liwale kuna
malalamiko ya wananchi kukosa dawa katika hospitali yetu, Mkuu wa Wilaya
kafuatilie huko Halmashauri ili kujua wanapeleka wapi fedha za dawa.”
Katika
bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
ya mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 236 zimetengwa
kwenye ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi alisema hali ya
upatikanaji wa dawa muhimu kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 iliongezeka
kwa asilimia 50 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2015/2016.
Bw.
Zambi alisema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka 2016 hadi Februari
2017 mkoa wa Lindi ulipokea sh milioni 538 kwa ajili ya ununuzi wa dawa
kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
“Hospitali
ya mkoa ilipokea sh. milioni 195,328,186 kwa ajili ya ununuzi wa dawa
na pia ilitumia sh. Milioni 127,171,700 toka fedha za uchangiaji kwa
ununuzi wa dawa.”
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wa Halmashauri kwenda
vijijini na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa utunzaji wa mazingira ili
kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Pia
amewaagiza Maofisa Kilimo wote kuhakikisha wanaacha kushinda maofisini
na badala yake waende mashambani kwa ajili ya kuwaelimisha wakulima
namna bora ya kulima kwa kufuata njia za kisasa ili kupata tija.
Kila ofisa kilimo awe na shamba lake ambalo litatumika kama darasa kwa wananchi
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,