Urusi yadaiwa kudukua vitalu vya nyuklia vya Marekani
Wadukuzi
wanaosadikika kuwa ni kutoka Urusi wamejaribu kudukua makumi ya vitalu
vya nyuklia vya Marekani katika mwezi Mei na Juni, kwa mujibu wa ripoti
ya vyombo vya usalama vya Marekani.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Ulinzi ya Homeland ya
Marekani (DHS), wadukuzi hao waliweka hatari kubwa kwenye vitalu hivyo
vilivyopo Kansas.
Hata
hivyo, vyombo vya ulinzi vya marekani na idara hiyo vilikataa kueleza
kwa undani endapo vitalu hivyo vya nyuklia vilidukuliwa au udukuzi
uliishia kwenye majaribio.
DHS
wamesema wanalihusisha tukio hilo na wadukuzi wa Urusi kwani mbinu
iliyotumika ni sawa na ile iliyotumika katika uchaguzi wa marekani
pamoja na udukuzi wa vitalu vya nyuklia vilivyoleta madhara makubwa
nchini Ukraine.
Idara
hiyo ilieleza kuwa wadukuzi waliwatumia barua pepe maafisa wa ngazi za
juu wa idara hiyo zilizosomeka ‘maombi ya kazi’, lakini zilikuwa
zimebeba ‘codes’ ambazo zingewawezesha kufanya udukuzi huo baada ya
maafisa hao kuzifungua.
Hata hivyo, msemaji wa DHS, Jenny Hageman alisema kuwa wadukuzi hao hawakuathiri utendaji wa vitalu hivyo.
“Ni
kweli kwamba hawakuleta madhara kwa sababu mfumo wa kompyuta
zinazotumika kwenye utendaji ni tofauti kabisa na mfumo mkuu,” Reuters
imemkariri Hageman.
Marekani
iliwahi kuituhumu Urusi kwa kufanya udukuaji kwenye vitalu mwaka 2015
vilivyopelekea kukatika kwa umeme katika nchi yote ya Ukraine.
Tuhuma
za udukuzi dhidi ya Urusi zimetolewa saa chache baada ya Rais wa
Marekani, Donald Trump kukutana kwa mara ya kwanza na Rais wa Urusi,
Vladimir Putin nchini Ujerumani walipokuwa wakihudhuria kikao cha G20.