TETEMEKO LA ARDHI LATOKEA KARAGWE KAGERA LEO JUMAPILI JULAI 30
Tetemeko lililodumu kwa takriban sekunde tano limetokea leo, Julai 30
saa nne asubuhi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kayanga wilayani Karagwe,
lakini hakuna madhara yaliyoripotiwa kutokea.
Ofisa wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Gabriel Mbogani amesema ili kupata
uhakika wa tetemeko hilo ni lazima kukusanya taarifa kwenye mitambo.
Amesema wananchi mkoani Kagera kwa sasa wapo makini baada ya kupatiwa
semina kutokana na tetemeko la Septemba mwaka jana ambalo lilisababisha
madhara makubwa.
“Wananchi wa Bukoba baada ya semina tulizotoa na kuwaonyesha ramani ya
matukio ya tetemeko wamekuwa na uelewa, hivyo hata likitokea dogo kiasi
gani lazima watoe taarifa,” alisema Mbogani.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa
haijulikani ni muda gani tetemeko kubwa linaweza kutokea kwa kuwa uzoefu
ni kuwa huanza dogo na baadaye kuwa kubwa.
Mkazi wa mji mdogo wa Kayanga, Elieth Kikaka amesema alitoka nje ya
nyumba baada ya tetemeko hilo kwa kuwa yamekuwa yakitokea mara kwa mara
mkoani Kagera hivyo linapotokea ni lazima kuchukua tahadhari.