TCRA yapiga marufuku matangazo kwenye miito ya simu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imepiga marufuku matangazo ya biashara yanayowekwa mtumiaji anapopiga simu ili kutoa fursa kwa watumiaji kupata mawasiliano bila usumbufu.
Mkurugenzi wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amesema jana (Ijumaa) kuwa mamlaka hiyo imepokea malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa simu wakilalamikia matangazo hayo yanayotolewa na kampuni za simu.
Amesema tayari TCRA imeshaziandikia barua kampuni zote za simu kusitisha matangazo hayo na itakutana nazo kwa majadiliano ya kina Julai 6.
Amesema mamlaka haitambui utaratibu huo na inauchukulia kama kero kwa watumiaji wa simu ambao hutegemea kutumia njia hiyo ya mawasiliano kurahisisha mambo.
“Tuna imani mtu anapopiga simu ana shida ya haraka na anahitaji afanye mawasiliano, unapomuwekea matangazo kwa dakika tatu au nne ni usumbufu,” amesema.
Katika siku za karibuni imekuwa ni kawaida kwa mtu anayepiga simu kusikiliza wimbo au matangazo ya biashara na baadaye kuambiwa namba anayopiga haipatikani.