Serikali kuiunganisha mikoa ya Rukwa na Songwe
Serikali
imesema kuwa itaanza kujenga daraja la Mto Momba litakaloiunganisha
Mikoa ya Rukwa na Songwe kwaajili ya kuondoa kero kwa wananchi ambayo
imekuwa ikiwasumbua hasa wakati wa masika.
Hayo
yamesemwa Naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin
Ngonyani mara baada ya ziara ya ukaguzi wa barabara Kasansa mpaka
Kilyamatundu ambapo amesema kuwa tayari Serikali imeshampata mkandarasi
atakayejenga daraja hilo.
“Serikali
imeshatoa kiasi cha sh. Bilioni tatu fedha hizo zimetusaidia kutangaza
zabuni na kumpata mkandarasi, tayari Mkandarasi wa ujenzi huu
ameshapatikana na mkataba wa makubaliano ya ujenzi umeshakamilika hivyo
mkandarasi atausaini rasmi hivi karibuni,” amesema Eng. Ngonyani.
Aidha,
Eng.Ngonyani amesema kuwa ujenzi na kukamilika kwa daraja hilo
kutasaidia kukuza uchumi na wa wananchi wa mikoa hiyo, hivyo kuongeza
pato la taifa wakati huu nchi inaelekea kwenye uchumi wa kati wa Viwanda
Vile
Vile amemuagiza Meneja Wa Wakala wa barabara (TANROADS) Mkoa wa Rukwa
kuhakikisha anatoa ajira kwa wakazi waliopo kata ya Kipeta ambapo ujenzi
wa daraja hilo utafanyika.
Hata
hivyo, kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kwela, Ignas Malocha
ameishukuru Serikali ya awamu ya tano ya Dkt. John Magufuli kwa
kutekeleza ahadi ya ujenzi wa daraja hilo ambalo kukamilika kwake
kutawaletea maendeleo wakazi hao kwa vile litaufungua Mkoa wa Rukwa na
kuunganisha na Songwe na Katavi.
Naye
meneja wa TANROADS Rukwa Eng. Msuka Mkina amewahakikishia wakazi kijiji
cha Kilyamatundu kuwa Wakala utasimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa
wakati na viwango na kupitia mradi huo wananchi hao watapata ajira.