Serikali Kuendelea Kuboresha Mazingira Ya Kuabudu Nchini
Na Dotto Mwaibale
SERIKALI
itaendelea kuboresha mazingira bora na wezeshi ili kila mtanzania apate
uhuru wa kuabudu kupitia dini yake na hata kwa yule ambaye hana dini.
Hayo
yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ,
Angela Kairuki wakati akihutubia kwenye maaombi maalumu ya kitaifa ya
kuombea nchi na Rais Dk.John Magufuli yaliyofanyika Uwanja wa Uhuru
jijini Dar es Salaam jana ambapo alikuwa mgeni rasmi.
“Serikali
licha ya kuwa haina dini itaendelea kuboresha mazingira ya kuabudu ili
kila mwananchi apate fursa ya kuabudu bila ya bugudha yoyote” alisema
Kairuki.
Alisema
viongozi wa dini kuptia taasisi zao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya
kuiletea nchi maendeleo na amani ambayo imedumu tangu tupate uhuru hivyo
wanapaswa kupongezwa.
Kairuki
alisema serikali ina thamini maombi yanayofanywa na viongozi wa dini
hapa nchini kwani yanaleta amani, umoja na uzalendo na si kwa waumini wa
dini pekee bali na kwa watu wote wenye mapenzi na nchi yetu.
Waziri
Kairuki alisema ni vizuri tukatumia fursa hii ya amani iliyopo nchini
kwa kila mtu kufanya kazi kwa bidii kama Rais Dk.John Magufuli
anavyohimiza kila siku ikiwa pamoja na kumuombea.
Mtumishi
wa mungu muhubiri wa kimataifa mtanzania anayeishi Marekani, Dk. Nicku
Kyungu ‘Mama Afrika’ ambaye alipata maono ya kufanya mkutano huo wa
maombi ya shukrani hapa nchini alisema Afrika pamoja na Tanzania
zimebarikiwa kwa kuwa na rasilimali za kutosha tulizopewa na mungu hivyo
hatuna budi kumshukuru mungu.
Alisema
Tanzania imejaa kila kitu kizuri, mbuga za wanyama, madini, ardhi
ikiwemo amani iliyodumu tangu utawala wa Hayati baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na
sasa Dk. John Magufuli.
Alisema
kutokana na neema hiyo kutoka kwa mungu aliona ni vema yakafanyika
maombi ya shukrani ya kitaifa na kumuombea Rais Dk.John Magufuli na nchi
kwa ujumla.
Dk.Kyungu
alisema kauli alioianzisha Rais Dk. Magufuli ya Hapa Kazi tu ipo katika
biblia hivyo ni wajibu wa kila mtu kufanya kazi kama mungu
alivyomuagiza adamu pale bustani ya hedeni na hiyo itasaidia kupambana
na adui umaskini, ujinga na maradhi hasa katika kipindi hiki ambacho
Rais Dk. John Magufuli anahimiza nchi kuingia katika uchumi wa viwanda.
Katika
maombi hayo maaskofu wakuu zaidi ya kumi kutoka ndani na nje ya
Tanzania waliweza kuiombea nchi katika maeneo mbalimbali, kama uchumi,
vyama vya siasa na viongozi wao, Rais na Serikali, Bunge, amani, masuala
ya ulinzi na usalama na mambo mengine.
Maombi
hayo ambayo ni ya kihistoria hapa nchini yaliandaliwa na viongozi wa
dini kutoka madhehebu ya Huduma ya Kikristo Tanzania na Taasisi ya I Go
Africa For Jesus yalifanyika kuanzia saa nne asubuhi hadi jioni na
kuhudhuriwa na mamia ya watanzania na viongozi wa dini huku yakipambwa
na burudani za nyimbo za kumtukuza mungu kutoka kwaya mbalimbali ambapo
yalifungwa na neno la shukrani na Mratibu wa maombi hayo ambaye ni
Askofu Mkuu wa Kanisa la Abudant Blessing Center (ABC), Askofu Flaston
Ndabila.
Baadhi
ya maaskofu wakuu waliohudhuria maombi hayo ni pamoja na Dk. Philemon
Tibananason, Dk.Bernard Nwaka kutoka Zambia, Sylvester Gamanywa,
Lawrence Kameta, Dk.Barnabas Mtokambali, Timoth Joseph kutoka Nigeria na
wengine kutoka nje ya nchi.