REA AWAMU YA TATU YAZINDULIWA SIMIYU, VIJIJI 347 KUPATA UMEME
Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Mhe.Dkt.Medard Kalemani (mwenye suti nyeusi katikati) akikata utepe kabla ya
kuzindua Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu katika
Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima
Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Mhe.Dkt.Medard Kalemani akizindua Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu
Mkoani Simiyu katika Kijiji cha Nangale wilayani Itilima (kushoto) Mkuu wa mkoa
huo, Mhe.Anthony Mtaka.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Medard Kalemani akiwaonesha wananchi Kifaa kiitwacho UMETA(Umeme Tayari) ambacho hutumika kuleta nishati ya umeme katika nyumba ambazo haziwezi husukwa nyaya wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima |
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya
Itilima wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard
Kalemani(hayupo pichani) wakati wa wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme
Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu katika Kijiji cha Nangale wilaya ya
Itilima.
|
Jumla ya Vijiji 347 Mkoani Simiyu vinatarajia kupata Umeme
kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya Tatu ambao utatekelezwa katika
kipindi cha miezi 24 kuanzia mwezi Julai 2017.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Mhe.Dkt.Medard Kalemani wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)
Awamu ya Tatu na utambulisho wa Mkandarasi wa mradi katika Kijiji cha Nangale,
Kata ya Ndolelezi Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.
“Mradi wa REA awamu ya tatu utapeleka Umeme katika vijiji
vyote vya Mkoa wa Simiyu hilo la kwanza, pili mradi huu utapeleka Umeme katika
vitongoji vyote hata vijiji ambavyo vilipelekewa Umeme lakini baadhi ya
vitongoji vyake bado havina, katika awamu hii navyo vinapelekewa” amesema
Kalemani.
Ameongeza kuwa Umeme wa REA awamu ya
tatu pamoja na kuwanufaisha wananchi katika makazi yao kwenye vijiji vyote 347 vilivyosalia
pia utapelekwa katika Taasisi za Umma zikiwepo shule, vituo vya kutolea huduma
za afya, visima na mitambo ya miradi ya maji pamoja na nyumba za ibada(
makanisa na misikiti).
Akimkabidhi Mkandarasi wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu ambaye
ni Kampuni ya JV White City International kwa Wananchi wa Mkoa wa Simiyu,
Dkt.Kalemani amemtaka kuhakisha kuwa anatekeleza mradi ndani ya
muda uliopangwa (miezi 24), akiwatumia wakandarasi wasaidizi wenye sifa kutoka
ndani ya mkoa na kuwapa ujira wao kama inavyotakiwa pamoja na kununua
vifaa vyote zikiwemo nguzo na transifoma hapa nchini.
Amemtaka Meneja wa TANESCO Mkoa wa
Simiyu, Mhandisi Rehema Mashinji kusimamia na kuhakikisha kuwa wakandarasi
watakaowaunganishia wananchi Umeme ni wale walioidhinishwa na shirika hilo ili
kuepuka Vishoka ambao watawaongezea wananchi gharama zisizo za lazima.
HABARI NA PICHA NA COSTANTINE MATHIAS SIMIYU