Rais Magufuli Atoa Onyo Kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaonya
wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kote nchini na kuwataka kuwa na
nidhamu ya pesa na kutumia fedha za serikali vizuri.
Rais
Magufuli amesema hayo leo wilayani Chato mkoani Geita alipokuwa
akihutubia wananchi katika makabidhiano ya nyumba 50 zilizojengwa na
taasisi ya Benjamin Mkapa, ambapo mbali ya kushukuru kwa msaada huo Rais
Magufuli alizungumzia juu ya tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali
kuiba fedha za wananchi na kutumia katika mambo yao wenyewe nje ya
malengo ya serikali.
"Hapa
penyewe Chato kuna fedha zaidi ya bilioni moja za pembejeo zimeliwa na
viongozi, hivyo natoa wito kwa viongozi wote wakuu wa wilaya na wakuu wa
mikoa kote nchini kuwa na nidhamu na fedha za serikali, tujifunze
kutumia fedha vizuri za serikali asitokee mchwa huko kula pesa za
serikali. Maana hili lililotokea hapa Chato najua limetokea sehemu
nyingi na hivyo saizi tunaanza kufanya ukaguzi kila sehemu" alisema Rais Magufuli
Mbali
na hilo Rais Magufuli aliwataka wananchi wa hali ya chini kuwa na amani
kwani katika kipindi chote ambacho yeye atakuwa madarakani hataki kuona
wala kusikia wananchi wa hali ya chini wakinyanyaswa sababu na yeye
ametokea katika maisha hayo hivyo anatambua jinsi wanavyopata shida watu
wa kipato cha chini.
"Serikali
haiwezi kufanya biashara na masikini, inawaacha matajiri inawasumbua
masikini, mimi nimekuwa katika maisha ya shida nimechunga ng'ombe,
nimeuza maziwa kwa hiyo najua maisha ni nini. Najua Tanzania watu wengi
wanaishi maisha ya chini na katika kipindi changu sitaki kuona watu wa
hali ya chini wanapata shida, wanapata taabu ndiyo maana tunajitahidi
kuhangaika kuleta maendeleo ili wanufaike na wao" alisisitiza Magufuli
Rais
Magufuli akuziacha taasisi ambazo zimekuwa zikitetea wanafunzi kupata
mimba na kusema yeye taasisi hizo hazipendi na ameziwekea kizingiti kuwa
ikiwezekana zisipewe msaada bali taasisi zinazofanya mambo ya
kimaendeleo kama taasisi ya Mkapa Foundation ndiyo zinatakiwa kupewa
msaada sana kwa kuwa zinarudi kuleta maendeleo kwa wananchi.