Polepole: Lowassa Sio Tishio kwa CCM......Amechuja na Akigombea Tena 2020 Tutamshinda
Siku
moja baada ya mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa kusema
atagombea tena urais katika uchaguzi ujao, CCM imesema inamsubiri na ina
uhakika itamshinda tena kwa kuwa tayari ameshachuja na wala sio tishio.
Lowassa
aliweka rekodi ya kuwa mgombea wa upinzani aliyepata kura nyingi baada
ya kugombea kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vingine
vitatu vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Alipata
kura milioni 6.07, takriban mara tatu ya kura ambazo wapinzani wamekuwa
wakipata katika chaguzinne za awali. Mshindi alikuwa John Magufuli wa
CCM aliyepata kura milioni 8.8.
Waziri
huyo mkuu wa zamani ametangaza nia ya kusimama tena kugombea urais
wakati alipofanya mahojiano na waandishi wa Nation Media Group jijini
Nairobi, Kenya ambako alikwenda kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa waziri
wa mambo ya ndani, lakini CCM imesema asitarajie ushindi.
Alipoulizwa
kuhusu tamko la Lowassa, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey
Polepole alisema mbunge huyo wa zamani wa Monduli si tishio na hayuko
katika fikra za chama hicho.
“Katika orodha ya vitu muhimu, Lowassa hatumfikirii kabisa na si tishio hata kidogo,” alisema Polepole ambaye katika uchaguzi uliopita aliapa kuzunguka nchi nzima kumpinga Lowassa.
Polepole
alisema kwa sasa chama hicho kimejikita kutekeleza Ilani yake
inayotokana na ahadi za wananchi, kama kushughulikia changamoto za
uadilifu kwa viongozi ndani ya CCM na Serikali.
“Tunatimiza
wajibu wetu vizuri tuliotumwa na Watanzania na kazi inaonekana. Nje ya
hapo tunasubiri Watanzania watupatie haki yetu katika uchaguzi ujao, na
tumeshajipangia kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 70, kwa hiyo
hatumfikirii kabisa,” alisema Polepole.
Hata
hivyo, jina la Lowassa limekuwa gumzo katika vikao vya chama hicho
tawala na alisababisha wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya CCM kuchukuliwa
hatua, wenyeviti wanne wa mikoa kuvuliwa uongozi na uanachama na wengine
kadhaa kuadhibiwa kwa njia tofauti.
Hiyo
ilitokana na baadhi kuendelea kumuunga mkono baada ya kujivua uanachama
wa CCM na kujiunga upinzani, akiwa Waziri Mkuu wa kwanza kufanya hivyo
tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992.