Ngeleja Aeleza kwanini hakumrudishia fedha za Escrow Rugemalira na Badala yake Alizipeleka TRA
Siku
chache baada ya kutangaza kuwasilisha shilingi milioni 40 katika
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja
amefafanua sababu za kutomrejeshea fedha huyo mfanyabiashara, James
Rugemalira ambaye alimpa awali kama msaada.
Fedha
hizo ni sehemu ya shilingi bilioni 306 zilizotolewa katika akaunti
maalum ya Tegeta Escrow mwaka 2014 iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania,
fedha zizotolewa kimakosa wakati kesi ya mgogoro wa kati ya Tanesco na
Kampuni ya kufua umeme ya IPTL ikiwa bado haijatolewa maamuzi.
Kwa
mujibu wa taratibu, fedha hizo zilipaswa kutolewa baada ya kesi husika
kukamilika na pande zote mbili kukaa pamoja kukokotoa kiasi cha fedha
ambacho kila upande ungepaswa kupata kwa mujibu wa maamuzi.
“Kwa
mazingira halisi yanayomkabili aliyenipa msaada, mahali salama pa
kurejesha hizo fedha sasa ni serikalini. Serikali itajua kuwa fedha hizo
zinastahili kwenda kwa Rugemalira sasa au wasubiri hatima ya kesi,” Ngeleja anakaririwa na Gazeti la Mwananchi .
“Ningerudisha kwa Rugemarila watu wangeweza kuibua hoja kwamba labda napiga changa la macho tu,” aliongeza.
Mfanyabiashara
huyo maarufu ambaye kampuni yake ya VIP Engineering ilikuwa inamiliki
asilimia 30 ya IPTL, pamoja na Mwenyekiti wa Pan African Power Solution
(PAP), Harbinder Singh Seth wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na
bado wako mahabusu.
Mgao
wa fedha hizo pia uliwafikia Anna Tibaijuka aliyekuwa waziri wa Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Andrew Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Methodiu Kilaini, Jaji
John Ruhangisa na wengine.