MKE WA MTU AJIUA KWA KUJINYONGA KISA AMESHINDWA KUREJESHA PESA ZA MKOPO SHINYANGA
Mkazi wa mtaa wa Tambukareli kata ya
Ndembezi katika manispaa ya Shinyanga Sarah Bundala (55) amejiua kwa
kujinyonga kutokana na kile kilidaiwa kuwa ameshindwa kurejesha fedha za
mkopo alizomdhamini rafiki yake ambaye ametoroka.
Pesa alizotoroka nazo rafiki huyo hazijulikani idadi yake.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani
Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro alithibitisha kutokea kwa tukio hilo
lililotokea jana Ijumaa Julai 14,2017.
Akizungumzia tukio hilo mume wa marehemu
Laurent Mabina, alisema wakati akiwa bado kazini majira ya saa 9 mchana
alipigiwa Simu na mke wake akimuomba Shilingi 40,000/- akamjibu kuwa
anarejea nyumbani muda huo na akifika wataangalia cha kufanya lakini
alipofika akakuta mkewe amejinyonga.
“Mke wangu alishawahi kukopa fedha
akashindwa kulipa nikalazimika kulipa na kumuonya kwamba asijiingize
tena kwenye masuala ya mikopo,huenda sababu ya mke wangu kujinyonga ni
ile hofu kuwa nikirudi nyumbani nitakuja kugombana naye sababu
nilishamkataza mambo ya mikopo" alisema Mabina.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa marehemu alikuwa amedhamini
rafiki yake apate mkopo lakini rafiki huyo akatoroka na pesa za mkopo
ambazo kiasi chake hakijafahamika hivyo deni la mkopo kuwa lake huku
wanaodai wakisema watafika nyumbani kumfirisi.
Akisimulia kuhusu tukio hilo rafiki yake Mariam Mgaya,aliiambia Malunde1
blog kuwa,majira ya saa nane mchana siku ya tukio alimuita ili
amsindikize wakatafute pesa za kukopa, ili akarejeshe marejesho lakini
walivyozunguka na kukosa ndipo akamshauri ampigie simu mume wake
amsaidie kiasi hicho cha pesa anachohitaji akagoma kufanya hivyo.
Alisema baada ya kushauriana wapi watapata pesa na kukosa majibu,
marehemu alimwambia anataka kwenda nyumbani kulala kwanza na ikifika
majira ya saa 10 arudi kumuona na hata watu wakimuuliza yuko wapi
awaambie amelala nyumbani kwake asiwafiche na ilipofika muda huo
akapokea taarifa rafiki yake amejinyonga.
Matukio ya watu kuchukua uamuzi wa kujiua yameanza kukithiri katika
manispaa ya Shinyanga ambapo ndani ya miezi miwili,Juni na Julai mwaka
huu,hili ni tukio la tano,matukio ambayo yanatokea katika kata ya
Ndembezi na Ngokolo ambazo zinatenganishwa na barabara ya Mohammed Trans
mjini Shinyanga.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog