Maofisa CDA wapangiwa kazi nyingine......Ni Baada ya Rais Magufuli Kuivunja
Wafanyakazi 260 wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Mji wa Dodoma (CDA) wamepangiwa vituo vipya vya kazi.
Kwa
mujibu wa Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene wafanyakazi 150 kutoka kundi hilo
wanabaki Manispaa ya Dodoma huku wengine 66 wakipelekwa katika
halmashuri na mikoa mbalimbali nchini.
Amesema
wafanyakazi 16 wamepelekwa Tamisemi, DART (14), Hospitali ya Benjamini
Mkapa Dodoma (4), Chuo Kikuu cha Dodoma (3), Ofisi ya Waziri Mkuu (3),
Wizara ya Ardhi (2) Ofisi ya Bunge (1) na Utumishi wa Umma (1).
Waziri
Simbachawene amewataka wafanyakazi hao kuripoti katika vituo vyao vya
kazi mara baada ya kupata barua na Serikali haitasita kufuta ajira ya
mtumishi yeyote ambaye atakaidi agizo hilo.
Rais
wa John Magufuli aliivunja rasmi CDA Mei mwaka huu na kuagiza mali na
shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na CDA zihamishiwe Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma.
Rais
Magufuli alisema ameamua kuivunja CDA na kuhamishia majukumu yake
katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa
utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alisema mkanganyiko huo ulikuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili.
Aidha, alisema mahitaji ya sasa yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya kuwepo kwa CDA.
“Wananchi
wa Dodoma wamelalamikia tatizo hili kwa muda mrefu, hata nilipokuwa
kwenye kampeni zangu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 walilalamika sana,
sasa nimetekeleza niliyowaahidi,” alisema Dk Magufuli.
“Naamini
kwa uamuzi huu malalamiko ya wananchi yatapata utatuzi na pia tutakuwa
tumeondoa kikwazo cha umiliki wa muda mfupi wa ardhi uliosababisha
wawekezaji kushindwa kujenga viwanda Dodoma.
CDA ilianzishwa kwa Amri ya Rais ya Aprili Mosi, 1973 na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230.